Mfanyibiashara Jimal Rohosafi atarajia mtoto wa kwanza na mridhi wa Amira na Amber Ray

Michelle alidokeza kuwa uhusiano wao umedumu zaidi ya mwaka mmoja.

Muhtasari

•Siku ya Jumanne, mfanyibiashara huyo mashuhuri alifichua kuwa anachumbiana na rafiki yake wa siku nyingi,  Michelle Thiong'o.

•Michelle alibainisha kuwa kupata mtoto pamoja ni uamuzi bora ambao aliwahi kufanya na mpenziwe.

Image: INSTAGRAM// JIMAL ROHOSAFI NA MICHELLE THIONG'O

Mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa Matatu Jimal Marlow Rohosafi amethibitisha kuwa yuko kwenye mahusiano mapya.

Siku ya Jumanne, mfanyibiashara huyo mashuhuri alifichua kuwa anachumbiana na rafiki yake wa siku nyingi,  Michelle Thiong'o.

Jimal alichapisha picha yake na Michelle ambaye alionekana kuwa mjamzito, dokezo kwamba wanatarajia mtoto wao wa kwanza pamoja.

"Nilisema nitapenda baada ya miaka mitatu na nikama imenda haraka.❤️ #hiimenda," aliandika chini ya picha hiyo.

Kwa upande wake, Michelle alibainisha kuwa kupata mtoto pamoja ni uamuzi bora ambao aliwahi kufanya na mpenziwe.

Pia alidokeza kuwa uhusiano wao umedumu zaidi ya mwaka mmoja huku akisherehekea siku ya kumbukumbu ya mahusiano yao.

"Tunasherehekea zaidi ya Siku yetu ya Wapendanao, uamuzi bora zaidi ambao tumewahi kufanya ni kuwa na wewe ❤️. #happyanniversary mpenzi wangu," Michelle aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Katika chapisho la awali, malkia huyo aliweka wazi kwamba alitaka kupata mtoto hata kabla ya kubeba ujauzito.

Jimal alitemwa na aliyekuwa mkewe, Amira, mwishoni mwa mwaka 2021 baada ya kuhusika kwenye mzozo wa mapenzi kwa muda mrefu. Baada ya kumtema mfanyibiashara huyo, Amira alielekea mahakamani kudai talaka.

Mwezi Julai mwaka jana, Jimal alikiri kujuta sana kwa kusababisha kuvunjika kwa ndoa yake na kuomba msamaha kutoka kwa Amira.

Mfanyibiashara huyo  alikiri kuwa alimkosea sana mama huyo wa watoto wake wawili kwa kuingiza drama nyingi kwenye ndoa yao.

"Naomba radhi kwa kukukosea heshima, kukuaibisha, kwa kukuumiza, kwa maumivu yote na kwa huzuni niliyokuletea. 💔Samahani kwa nyakati zote ambazo sijawa mwanaume niliyeahidi kuwa," alisema.

Pia alikiri kuwa alikosa kutimiza  wajibu wake wa kumlinda mkewe kama alivyohitajika kufanya. Alisema kwamba alifahamu wakati ndoa yake ikiporomoka ila akashindwa na la kufanya kwa wakati ule.

"Ilikuwa mbaya kabisa. Huenda nilionekana kama mtu asiye na wasiwasi lakini sikuwa na la kufanya. Nilijua haikuwa sawa, nilijua unaumia lakini sikuweza kujikusanya!Amira nafanya hivi kwa sababu ukosefu wa heshima pia ulikuwa mkubwa. Naomba radhi kwa kukosa heshima," Aliandika.

Jamal pia alikiri kwamba hajakuwa sawa tangu alipokosana na mke huyo wake na mama ya watoto wake.

Katika jibu lake kwa ombi hilo la msamaha Amira hata hivyo alidokeza kuwa anahitaji muda kwani "vidonda vingine haviponi."

Ndoa ya wawili hao ilianza kuporomoka baada ya Jimal kumchukua mwanasoshalaiti Amber Ray kama mke wa pili.