Jalango afichua kwa nini Kibe alishindwa katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Lang’ata 2013

"Hizo kura ziko huko kwa kijiji. Ulikuwa unapiga kampeni kwa baa," Jalang'o alimwambia Kibe.

Muhtasari

•Kibe na Jalang'o walijadili masuala mbalimbali kuanzia urafiki wao, taaluma siasa, hali ya taifa miongoni mwa mada nyinginezo.

•Kibe alikiri kwamba alisherehekea sana uvumi ulipoibuka kwamba Jalang'o ameshindwa kunyakua kiti hicho.

Jalang'o na Andrew Kibe
Image: HISANI

Siku ya Jumatano, mtumbuizaji Andrew Kibe na mbunge wa Lang'ata Phelix Odiwour almaarufu Jalang'o walishiriki mazungumzo ya moja kwa moja mtandaoni.

Wawili hao walijadili masuala mbalimbali kuanzia urafiki wao, taaluma zao, siasa, hali ya taifa miongoni mwa mada nyinginezo nyingi.

Katika mazungumzo hayo, Jalang'o alikuwa wazi kabisa kumfichulia mtumbuizaji huyo sababu iliyomfanya ashindwe kunyakua kiti cha ubunge cha Lang'ata ambacho yeye anakalia kwa sasa wakati wa jaribio lake mwaka wa 2013.

"Niliuliza kwa nini ulianguka kura. Walisema wewe Lang'ata yako ni hapo TNA, Onyonka, na maeneo hayo," alimwambia Kibe.

Mbunge huyo wa muhula wa kwanza alidokeza kwamba Kibe hana ufahamu mzuri wa mitaa yote katika eneo bunge la Lang'ata na alishindwa kwa sababu hakutembelea vitongoji mbalimbali  kwa ajili ya kuomba kura.

"Hizo kura ziko huko kwa kijiji. Ulikuwa unapiga kampeni kwa baa," Jalang'o alimwambia mtumbuizaji huyo.

Kibe kwa upande wake alimpongeza mbunge huyo wa ODM kwa ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Hata hivyo, alikiri kwamba alisherehekea sana uvumi ulipoibuka kwamba mtangazaji huyo wa zamani ameshindwa kunyakua kiti hicho katika jaribio lake la kwanza wakati wa hatua za awali za shughuli ya kuhesabu kura.

"Kwanza ukajua vile nilikuchekelea asubuhi vile niliskia umepoteza. Kaka, nilianguka hapa chini. Ungeniona. Nilikuwa nimesherehekea ati Jalas ameishi. Nilikuwa nimekufa,"  Kibe alimwambia mbunge huyo.

Jalang'o alisema alitazama video ya mtumbuizaji huyo akisherehekea kupoteza kwake na akapuuza tu akitamani pia yeye angekuwa katika kituo cha kuhesabu kura aweze kushuhudia kilichokuwa kikiendelea uwanjani.

Mwezi uliopita, Kibe alisema alikuwa tayari kwa kiti cha ubunge wa Lang'ata kabla ya ndoto yake kuangamizwa siku ya uchaguzi.

"Nilikuwa tayari sana. Nilipata, kama sijakosea, labda 1400. Unaweza kufanya nini na 1400 kwa sarafu yoyote," alisema.

Katika video, mtumbuizaji huyo alionyesha baadhi ya mabango ya kampeni aliyotumia kujipigia debe mwongo mmoja uliopita

Pia alionyesha cheti chake cha uteuzi cha UDF kilichomuidhinisha kuwania kiti cha ubunge wa Lang'ata kwa tikiti ya chama hicho.

"Tafadhali, kabla mniongeleshe. Weka heshima kwenye jina langu. Hii ni siku ambayo nilikuwa naenda kuchukua cheti changu kwa IEBC," Kibe alisema kuhusu picha iliyomuonyesha akiwa amevalia suti na kitambaa cha UDF.