Babu Tale ampandishia Diamond shinikizo la kumuoa 'mpenziwe' Zuchu

"Fanya basi uoe unanichelewesha ujue," alisema Babu Tale.

Muhtasari

•Diamond alimshukuru mwimbaji huyo wa kibao 'Sukari' kwa zawadi hiyo na kueleza jinsi anavyomthamini.

• Babu Tale alionekana kumshinikiza Diamond amuoe haraka malkia huyo kutoka Zanzibar.

katika ziara yao ya Ufaransa.
Diamond Platnumza na anayedaiwa kuwa mpenziwe, Zuchu katika ziara yao ya Ufaransa.
Image: INSTAGRAM// ZUCHU

Jumatano, staa wa Bongo Diamond Platnumz alionyesha mkufu wa thamani ambao alipewa na msanii wake Zuchu kama zawadi ya siku ya kuzaliwa.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diamond alimshukuru mwimbaji huyo wa kibao 'Sukari' kwa zawadi hiyo na kueleza jinsi anavyomthamini.

"Maneno hayawezi elezea shukran yangu kwa hili Zuuh.. nisije nikatereza kuandika waandishi wakapa kutoa stori bure, ila jua nakushukuru sana, na siku zote utaendelea kuwa pale," aliandika chini ya video ambayo alifuta muda mfupi baadae.

Katika video hiyo fupi, mastaa hao wawili wa Bongo walionekana wakikumbatiana kwa furaha na hata kwa wakati mmoja kubusu midomoni.

Kabla ya kufutwa, wanamitandao walijumuika chini ya chapisho hilo na kuandika maoni mseto kutokana na maudhui ya video hiyo.

Miongoni mwa walioacha jumbe zao chini ya chapisho lake ni pamoja na mmoja wa mameneja wake,Hamisi Shaban Taletale almaarufu  Babu Tale, ambaye alionekana kumshinikiza amuoe haraka malkia huyo kutoka Zanzibar.

"Fanya basi uoe unanichelewesha ujue," aliandika Babu Tale.

Babu Tale na Diamond Platnumz
Image: INSTAGRAM// BABU TALE

Diamond hata hivyo hakujibu ujumbe ule na badala yake aliifuta video hiyo ambayo ilikuwa imealika maoni mengi kwenye ukurasa wake.

Kwa muda mrefu Diamond na Zuchu wamekuwa wakiwakanganya mashabiki wao kuhusu uhusiano wao halisi.

Licha wa kuwa bosi wa Zuchu, Diamond pia amehusishwa na mwimbaji huyo kimapenzi huku wawili hao wakidaiwa kuwa wachumba.

Hapo awali bosi huyo wa WCB aliwahi kujitambulisha kama mume wa Zuuh, ila baadae binti huyo wa Khadija Kopa akajitenga na kauli hiyo.

"Zuuh wako wengi. Ni kweli naitwa Zuuh lakini si Zuuh mimi, kama ingekuwa mimi angeniambia. Itakuwa Zuuh mwingine," Zuchu alijibu.

Mara nyingi wawili hao wameonekana wakistarehe pamoja, wakijivinjari pamoja, wakicheza miondoko ya kimahaba jukwaani, wakisema maneno ya kimahaba kuhusu kila mmoja, kukumbatiana na hata kubusu.

Mwezi uliopita Zuchu alidokeza kuwa huenda hayupo tena kwenye mahusiano yoyote ya kimapenzi.

Single 😏 tena," Aliandika kwenye akaunti yake ya Snapchat.