Mwanamke Mkorino aliyedai alitungwa mimba na mapacha ampoteza bintiye wa wiki moja

Emily amepoteza mtoto wake mchanga wiki moja baada ya kujifungua.

Muhtasari

•Takriban wiki moja tu baada ya Emily kujifungua mtoto wa kike, Kui, mapacha hao walifichua kuwa mtoto huyo alifariki Alhamisi jioni.

•Ijumaa asubuhi, mapacha hao walizua drama nje ya Hospitali ya JM Kariuki wakidai majibu kuhusu kifo cha mtoto huyo wa wiki moja.

amepoteza mtoto wake wa wiki moja
Emily amepoteza mtoto wake wa wiki moja
Image: FACEBOOK// THE KIMATHIS

Mwanadada Mkorino ambaye alidaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mapacha wawili wa Nyandarua, Emily amepoteza mtoto wake mchanga.

Emily alikuja kuvuma kwenye mitandao ya kijamii mwaka jana baada ya kujitokeza akiwa  mjamzito na kudai kwamba hajui ni nani kati ya ndugu mapacha, Peter na Teddy ndiye baba halisi wa mtoto ambaye alikuwa amebeba tumboni.

Baadaye, mapacha hao hata hivyo  walijitokeza na kuweka mambo wazi huku akisema walikuwa wakitafuta kiki tu kutumia ujauzito huo.

Takriban wiki moja tu baada ya Emily kujifungua mtoto wa kike, Kui, mapacha hao walifichua kuwa mtoto huyo alifariki Alhamisi jioni. Walilaumu hospitali kwa kutomshughulikia mtoto huyo licha ya kuwa kwenye foleni kwa saa nyingi.

"Ukosefu wa pesa ulifanya tupoteze Kui tungeweza kukupeleka hospitali bora zaidi," taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Facebook wa mapacha hao ilisomeka.

Kulingana na taarifa hiyo, mtoto Kui alikuwa akisubiri kwenye laini kwa takriban saa tatu bila kuhudumiwa.

"Mapenzi ya Mungu, sio mimi wala Emily #RIPBABYKUI," mpenzi wa Emily aliandika baadaye kwenye ukurasa huo.

Mwanaume huyo aliyeonekana kuumia sana moyoni alibainisha kuwa ulikuwa wakati wa huzuni zaidi maishani mwake kumpoteza mtoto wake baada ya wiki moja tu ya kuwa naye.  Aidha, aliendelea kudai uboreshaji wa huduma za hospitali hiyo na kuwataka viongozi wa kaunti ya Nyandarua kuona hilo linafanyika.

Siku ya Ijumaa asubuhi, mapacha hao walizua drama nje ya Hospitali ya JM Kariuki wakidai majibu kuhusu kifo cha mtoto huyo wa wiki moja. Walidai kuwa marehemu alikuwa kwenye foleni kwa zaidi ya saa tano bila kuhudumiwa.