Nadia Mukami afunguka sababu ya kutengana na Arrow Bwoy

"Yeye ni baba ya mtoto wangu.Tumefungwa pamoja kwa maisha," alisema.

Muhtasari

•Nadia alisisitiza kuwa hatua ya kutangaza kusambaratika kwa ndoa yake mapema mwezi huu haikuwa kiki.

•Alidokeza kuwa alitengana na mwenza wake Arrow Bwoy baada ya kulemewa na mambo mengi ambayo yalitokea katika maisha yake.

Nadia Mukami na Arrow Bwoy
Image: HISANI

Malkia wa muziki wa Kenya Nadia Mukami amefunguka kuhusu kutengana na baba ya mtoto wake Ali Yusuf almaarufu Arrow Bwoy.

Katika mahojiano na Mungai Eve, Nadia alisisitiza kuwa hatua ya kutangaza kusambaratika kwa ndoa yake ambayo alichukua mapema mwezi huu haikuwa kiki.

Alisema kuwa kauli ambayo alitoa ndiyo aliyokusudia kusema na akaweka wazi kuwa watu wana haki ya kutafsiri jinsi wanavyotaka.

"Kulikuwa na maswali mengi kuhusu bookings na watu walikuwa wakiuliza maswali mengi ambayo singejibu kila mtu. Nilitoa taarifa tu, jinsi yeyote angetafsiri sio shida yangu," mama huyo wa mtoto mmoja alisema.

Nadia alibainisha kuwa licha ya kutengana kwao, bado ataendelea kumtambua mwanamuziki huyo mwenzake kama baba ya mtoto wake.

"Yeye ni baba ya mtoto wangu. Hilo halitabadilika.Tumefungwa pamoja kwa maisha. Imekuwa moja ya miaka ngumu zaidi kwangu," alisema.

Aidha, mwimbaji huyo alijitetea kwa yale yaliyotokea akisema kwamba yeye pia ni binadamu na ana hisia kama mtu mwingine yeyote.

"Watu husahau sisi ni binadamu. Nilijaribu kuwa mimi binafsi. Mimi sio mwenye drama." 

Mtunzi huyo wa wimbo 'Roho Mbaya' alidokeza kuwa alitengana na mwenza wake Arrow Bwoy baada ya kulemewa na mambo mengi ambayo yalitokea katika maisha yake katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Alikiri kwamba mambo mengi ambayo alikuwa akipitia wakati huo yalimsukuma kufikia hatua ya kuvunjika.

"Imekuwa moja ya miaka mbaya zaidi kwangu. Mungu amenibariki na pia nimepitia changamoto kwa viwango sawa. Nimepitia mengi, mambo yanaweza kuwa makubwa na inaweza kufikia mahali ukavunjika," alisema.

Aidha aliwasuta watu ambao walidai alikuwa akifanya kiki kwa ajili ya kutangaza biashara yake mpya ya urembo iliyofunguliwa jijini.

"Haiwezi kuwa mbinu ya kutangaza biashara. Iliikuwa ni sadfa tu. Watu wanaoweza kunielewa wanajua kwamba nimeolewa hivi majuzi, nimepata mtoto na inaweza kulemea mtu, utapanga virago, ni mambo mengi," alisema

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 26 alidokeza kwamba kuwa mama haijakuwa rahisi kwake na amekuwa akijaribu kusawazisha mambo mengi.

Nadia alithibitisha kutengana na Arrow Bwoy takriban wiki mbili zilizopita na kubainisha kuwa hawajakuwa pamoja kwa muda mrefu sasa.

Haya yalitokea takriban miezi tisa baada ya wasanii hao wawili kumkaribisha dunia mtoto wao wa kwanza, Haseeb Kai.