"Nimeishiwa na uwongo!" Nadia Mukami athibitisha kutengana na Arrow Bwoy

Alikiri kuwa ameshindwa kabisa kuendelea kudanganya kuhusu uhusiano wao.

Muhtasari

•Nadia Mukami alibainisha kuwa yeye na mzazi huyo mwenzake hawajakuwa pamoja kwa muda mrefu sasa

•Haya yanajiri takriban miezi tisa baada ya wasanii hao wawili kumkaribisha dunia mtoto wao wa kwanza, Haseeb Kai.

Nadia Mukami na Arrow Bwoy
Image: INSTAGRAM// NADIA MUKAMI

Malkia wa muziki wa Kenya Nadia Mukami amethibitisha kutengana na mwanamuziki mwenzake Arrow Bwoy.

Katika taarifa ambayo alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram, Nadia alibainisha kuwa yeye na mzazi huyo mwenzake hawajakuwa pamoja kwa muda mrefu sasa.

Alikiri kuwa ameshindwa kabisa kuendelea kudanganya kuhusu uhusiano wao kwa watu wengi ambao hawakuwa na ufahamu kuhusu kutengana kwao.

"Ili tu kuwafafanulia watu wanaojaribu kubook mimi na Arrow Bwoy, nimeishiwa na uwongo. Hatujakuwa pamoja kwa muda, tuliachana," Nadia Mukami aliandika kwenye Instastory zake siku ya Alhamisi.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 26 aliwataka watu wanaohitaji huduma zao za muziki kuwasiliana na usimamizi binafsi wa kila mmoja wao  na wakome kumtumia yeye na usimamizi wake kumfikia Arrow Bwoy.

Arrow Bwoy bado hajatoa taarifa yoyote kuhusu kutengana na Nadia kufikia kuchapishwa kwa makala haya.

Haya yanajiri takriban miezi tisa baada ya wasanii hao wawili kumkaribisha dunia mtoto wao wa kwanza, Haseeb Kai.

Nadia alijifungua mtoto wa kiume mnamo Machi 24 na kuthibitisha habari hizo kupitia ukurasa wake wa Instagam.

"Karibu katika ulimwengu wetu Haseeb Kai. Machi 24, 2022," Nadia aliandika chini ya picha iliyoonyesha akiwa amelala katika wodi ya uzazi na mumewe kando yake akiwa amemshika mtoto wao mikononi.

Arrow Bwoy alitaja mwanao kama zawadi nzuri kuwahi pokea maishani.

"24.03.2022 tumepokea zawadi nzuri zaidi Haseeb Kai. Karibu kwenye ulimwengu wetu," Arrow Bwoy aliandika.

Arrow Bwoy alimvisha Nadia pete ya uchumba mwezi Machi mwaka huu baada ya kuwa kwenye mahusiano kwa miezi kadhaa.

Tukio hilo la kupendeza lilitokea katika hafla ya uzinduzi wa albamu ya Arrow Bwoy 'Focus' ambayo ilifanyika Junction Mall.

"Sijui  niseme nini. Tumepitia mengi sana. Watu wamebonga sana. Wengine hawajaamini hadi wa leo yani.Nakupenda sana na ningependa kuishi maisha yangu yote nawe. Mpenzi wangu mrembo zaidi, mbele ya umati huu wote, je utakubali tufunge ndoa?" Arrow Bwoy alimwambia Nadia huku akiwa amepiga goti.

Mahusiano yao yalikuja kujikana hadharani mwaka uliopita.