Ukweli upi? Marioo adaiwa kutumana kwa Diamond abembelezwe amsaini WCB

Baba Levo amemtaka Marioo kukubali ukweli huku akimbainishia kwamba ni kitu cha zamani.

Muhtasari

•Diamond aliibua madai kwamba Marioo aliwahi kufika nyumbani kwake na kumuomba ampe nafasi katika lebo yake.

•Mwijaku hata hivyo amemshauri msanii huyo kutokubali kuyumbishwa kwani kulingana naye, kunao watu ambao wanataka apoteze mwelekeo wake.

Image: INSTAGRAM// MARIOO

Swali la iwapo staa wa Bongo Omary Mwanga almaarufu Marioo aliwahi kuwa katika hali mbaya  hadi kumpelekea kumfuata Diamond Platnumz amsaini katika Lebo ya Wasafi bado limesalia kuwa  kitendawili.

Diamond, katika mahojiano ya hivi majuzi alidai kwamba mwimbaji huyo ambaye ameendelea kuvuma katika siku za hivi majuzi aliwahi kufika nyumbani kwake na kumuomba ampe nafasi katika lebo yake.

"Kabla ya kutoa Beer tamu Marioo alikuja nyumbani. Alipokuja na tukazungumza alitaka nimsaini. Nilimwambia, Marioo nikikutazama naona unafanya vizuri, nahisi kama kukusaini sio kukutendea  haki maana wewe tayari unafanya vizuri. Nikikusaini unajua kuna watu wengine ambao wataleta chuki zao kwa sababu unafuatana na Diamond na wasikupigie nyimbo. Kuna radio nyingi ambazo hazipigi nyimbo zangu, watakuwa hawakupigii zako," alisema Diamond kwenye mahojiano.

Bosi huyo wa WCB alisema alimwagiza Marioo kutafakari kuhusu hatua hiyo na mazungumzo yao kabla ya kufanya uamuzi.

Aidha alisema kwamba aliahidi kumsaidia staa huyo wa Bongo katika matatizo yoyote aliyokuwa akipitia.

"Nilimwambia kama una matatizo aje ofisini tutampa hela.Tulizungumza vizuri na mdogo wangu Marioo akanielewa," alisema.

Marioo hata hivyo alijitokeza kupuuzilia mbali madai ya mwimbaji huyo mwenzake na kuyataja kuwa kuteleza kwa ulimi.

Alikuwa akimjibu mtangazaji na mchekeshaji mashuhuri wa Bongo Mwijaku ambaye aliuliza ukweli kuhusu madai hayo.

"Ongea kitu mashabiki zako tupoe. Ulikosa nini mpaka uliomba kwenda UCHAFUNI? Tuambie tujirekebishe," Mwijaku alihoji chini ya chapisho moja la mwimbaji huyo kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Marioo alijibu, "Hahaha Mkubwa kateleza, mfupa hauna ulimi😃."

Kufuatia hayo, msanii mkongwe wa Bongo ambaye pia ni mwandani wa Diamond, Baba Levo amejitokeza kumtetea huku akidai kuwa ni mara nyingi Marioo amemtuma kwa bosi huyo wa WCB kumuomba amsaini kwenye lebo hiyo maarufu.

"Mdogo Wangu Marioo Leo unakataa kwamba Haukuomba Kusainiwa na @diamondplatnumz!!? KWELI..!?Umenituma Mara Ngapi Nikakubembelezee Kwa @diamondplatnumz," aliandika kwenye mtandao wa Instagram.

Baba Levo na Diamond
Image: INSTAGRAM// BABA LEVO

Mwimbaji huyo mkongwe alimwomba Marioo kukubali ukweli huku akimbainishia kwamba ni kitu cha zamani.

Mchekeshaji na mtangazaji maaruufu wa Bongo Mwijaku hata hivyo amemshauri msanii huyo kutokubali kuyumbishwa kwani kulingana naye, kunao watu ambao wanataka apoteze mwelekeo wake.

"Huu ni mwaka wako, waombe poo ndio maana hata collabo wanaogopaa kuiachia. Wewe ni mkali kwa sasa," alisema.