Zari afunguka kuongeza watoto na mpenziwe Shakib baada ya kukutana na wazazi wake

"Shakib alinipeleka kuwaona wazazi wake na ilikuwa nzuri sana," Zari alisema.

Muhtasari

•Mwanasoshalaiti huyo ameweka wazi kuwa yuko tayari kupeleka mahusiano yake mapya katika kiwango cha juu zaidi.

•Zari pia alifichua kuwa anapanga kuongeza watoto zaidi na Shakib.

Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Mwanasosholaiti na mfanyibiashara mashuhuri Zari Hassan amepiga hatua ya kukutana na wazazi wa mpenzi wake Shakib Lutaaya.

Mpenzi huyo wa zamani wa staa wa Bongo Diamond Platnumz ameweka wazi kuwa yuko tayari kupeleka mahusiano yake mapya katika kiwango cha juu zaidi.

"Shakib alinipeleka kuwaona wazazi wake na ilikuwa nzuri sana," Zari alisema.

Mahusiano ya Zari na Shakib yamekuwa yakikosolewa sana hasa mitandaoni, suala kuu likiwa tofuati zao za umri. Zari ana umri wa miaka 42 ilhali mpenziwe alitimiza miaka 31 hivi majuzi.

Mama huyo wa watoto watano hata hivyo alibainisha kuwa wazazi wa Shakib hawakuashiria tatizo lolote na mahusiano yao na kubainisha kuwa mkutano wao ulikuwa mzuri.

“Alinipeleka kuonana na wazazi wake na walikuwa wazuri sana, na sikumbuki hata kidogo wakilalamika kuhusu uhusiano huo,” mzaliwa huyo wa Uganda alisema na kuongeza kuwa hatajitetea kabisa.

Zari pia alifichua kuwa anapanga kuongeza watoto zaidi na Shakib lakini akabainisha kuwa si kwa sababu ya shinikizo la umma.

Haya yanajiri takriban miezi mitatu baada ya mwanasoshalaiti huyo kudokeza kufunga pingu za maisha na Shakib baada ya kufichua kuwa mpenzi huyo wake wa sasa anapanga kupeleka posa kwa baba yake nchini Uganda.

"Shakib aliniambia jana kuwa anataka kukutana na baba yangu. Anataka kutoa posa kwa ajili ya ndoa, yuko tayari kunioa," Zari alisema kwa Kiganda  katika video ambayo ilipakiwa kwenye Snapchat mwezi Septemba.

Katika video hiyo fupi, mama huyo wa watoto watano aliendelea kuwatupia vijembe wakosoaji wa mahusiano yake na Bw Shakib huku akiwathibitishia kuwa juhudi zao kuwatenganisha zilikuwa zimefeli.

"Waliosema itaishia kwa machozi rudini kwa waganga wenu mkaombe warudishe hela, uchawi haukufanya kazi," alisema.

Kabla ya kujitosa kwenye mahusiano na Bw Shakib, mwanasoshalaiti huyo ambaye anaishi Afrika Kusini alichumbiana na mfanyibiashara wa Uganda aliyetambulishwa kama GK Choppa mapema mwaka huu.