Mtangazaji Jalang'o ajiuzulu kuingia siasa

Muhtasari

• Mtangazaji Phelix Odiwuor almaarufu Jalang'o amejiunga kwenye siasa baaday ya kuwa redioni kwa mara ya mwisho Februari 9.

• Mtangazaji huyo ambaye pia ni mchekeshaji alisema kwamba kuingia katika siasa imekuwa ndoto yake.

Jalang'o
Image: Instagram

Mtangazaji Phelix Odiwuor almaarufu Jalang'o amejiuzulu rasmi kutoka kazi ya utangazji ili kujitosa kwenye bahari ya siasa.

Jalang'o ambaye analenga kuania kiti cha eneo bunge la  Lang’ata amesema kwamba huu ulikuwa uamuzi mgumu ila lazima tu angechukua maamuzi ili kujaribu karata yake kwenye siasa kwa sababu anahisi ni wito.

“Nimeanza ukurasa mpya, rasmi naenda kujaribu bahati yangu katika siasa. Na huu ni mwito ambao nahisi kwamba, baada ya kuambiwa kwa muda mrefu kwamba vijana muda wenu unakuja", Jalang'o alisema.

Aliongeza kuwa ...  "Sisi si vijana tena na muda ambao tulikuwa tukiambiwa tusubiri tukiendelea kusubiri muda huo utapita. Huu ni kama wito kwangu ili kuenda kujaribu bahati yangu kwa kitu kipya kabisa”.

Mtangazaji huyo ambaye pia anajiongeza kama mchekeshaji alisema kwamba kuingia katika siasa imekuwa ni ndoto yake ambayo amekuwa akiwaza kuongoza watu na pia kujaribu na kuleta mabadiliko ili kuwaonesha watu kwamba viongozi wazuri bado wapo.

Ameshukuru uongozi mzima wa kampuni ya Radio Africa kwa kumuamini na kumpa nafasi kwa miaka kadhaa ambayo amehudumu kama mtangazaji katika shirika hili.

Jalango pia amemshukuru mtangazaji mwenza Kamene Goro kwa ushirikiano mkubwa uliofanikisha kipindi chao cha asubuhi kwenye redio ya Kiss100 kuwa kipindi maarufu Zaidi nchini Kenya.

Vile vile, mcheshi huyo amewashukuru wasikilizaji wote ambao wamekuwa wakilisukuma gurudumu la kipindi chao cha asubuhi, kuamka mapema na kuungana nao kwenye mitandao na kwenye redio zao.

Jalang'o anaondoka redioni ili kuwania ubunge wa Lang’ata jijini Nairobi, kuambatana na agizo la mamlaka ya mawasiliano nchini Kenya lililowataka watangazaji wanaolenga viti vya kisiasa kuachia ngazi kama watangazaji na wanahabari.