Orodha ya watu mashuhuri ambao wametangaza kuwania viti vya kisiasa mwaka wa 2022

Muhtasari

•Hapo awali mawakili na wafanyikazi katika afisi za umma ndio walionekana kufurika kwenye  siasa ila hivi majuzi tumeshuhudia wasanii na watu wengi mashuhuri wakitangaza azma ya kuwania viti vya kisiasa.

MC Jessy, Willy Paul, Jalang'o
MC Jessy, Willy Paul, Jalang'o
Image: INSTAGRAM

Siasa za Kenya zimeendelea kuchukua mikondo mipya huku sasa zikionekana kuvutia watu wengi kutoka tabaka, vitengo na  jamii mbalimbali.

Hapo awali mawakili na wafanyikazi katika afisi za umma ndio walionekana kufurika kwenye  siasa ila hivi majuzi tumeshuhudia wasanii na watu wengi mashuhuri wakitangaza azma ya kuwania viti vya kisiasa.

Katika makala haya tunaangazia baadhi ya watu mashuhuri ambao tayari wametangaza kuwepo debeni katika chaguzi za mwaka ujao.

1. McDonald Mariga

Mchezaji huyo wa zamani wa Harambee Stars aliwania kiti cha ubunge cha Kibra kwa tikiti ya Jubilee bila mafanikio katika chaguzi ndogo zilizofanyika mwaka wa 2019 baada ya aliyekuwa mbunge Ken Okoth kuaga dunia.

Licha ya kupoteza kiti hicho kwa Imran Okoth, Mariga hajapoteza nia yake kwa siasa na analenga kuwania tena mwaka ujao kwa tikiti ya UDA.

2. Felix Odiwour (Jalang'o)

Mchekeshaji mashuhuri Felix Odiwour almaarufu kama Jalang'o tayari ametangaza azma yake ya kuwania kiti cha ubunge cha Lang'ata mwaka ujao.

Jalang'o ambaye anawania kiti  hicho kwa tikiti ya ODM analenga kumtimua Nixon Korir wa Jubilee ambaye amekikalia kwa sasa.

3. Jasper Muthomi (MC Jessy)

Mchekeshaji wa Churchill Show na Churchill Raw Jasper Muthomi almaarufu kama MC Jessy anatazamia kuingia bungeni mwaka ujao.

Jessy ambaye ni mzaliwa wa kaunti ya Meru tayari ametangaza azma ya kuwania kiti cha ubunge cha Imenti Kusini.

4. Reuben Kigame

Mwanamuziki mashuhuri wa nyimbo za injili Reuben Kigame anatazamia kuridhi kiti cha urais kutoka kwa Uhuru Kenyatta mwaka ujao.

Mwanamuziki huyo ambaye ana ulemavu wa macho tayari ametangaza azma yake ya kuwania kiti cha urais. Atamenyana na wanasiasa wengine kama vile William Ruto, Raila Odinga Musalia Mudavadi na wengine.

5. Wilson Radido (Willy Paul)

Mwanamuziki wa nyimbo za kidunia Willly Paul ndiye msanii wa hivi  majuzi kutangaza azma yake ya kuwania kiti cha kisiasa.

Willy Paul alitangaza kuwania kiti cha ubunge cha Mathare siku ya Jumapili kupitia ukurasa wake wa Instagram.

6. Smith Mwatia (Rufftone)

Mwanamuziki wa nyimbo za injili Smith Mwatia almaarufu kama Rufftone sio mgeni kwa siasa. Hapo awali Rufftone amejihusisha katika masuala mbalimbali yanayogusia siasa ikiwemo kutunga nyimbo za kisiasa.

Rufftone ameonyesha nia yake ya kuwania kiti cha useneta katika kaunti ya Nairobi ambacho kwa sasa kimekaliwa na Johnson Sakaja.

7. Mwanaisha Chidzuga

Mtangazaji wa televisheni Mwanaisha Chidzuga alifanya maamuzi ya  kujitosa kwenye siasa mapema mwaka huu.

Chidzuga atawania kiti cha ubunge cha Matuga mwaka ujao.

8. Jamal Gaddafi

Mtangazaji Jamal Gaddafi tayari ametangaza azma yake ya kuwania kiti cha ubunge cha Malindi ambacho kwa sasa kimekaliwa na Aisha Jumwa.

9. Tabitha Karanja

Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi mwenza wa Kampuni ya Keroche Breweries amejitosa kwenye siasa za 2022, na kuzindua azma yake ya kuwania kiti cha useneta  cha  kaunti ya Nakuru.

10. Jackson  Makini  (Prezzo)

Mwanamuziki Jackson Makini almaarufu kama Prezzo alionyesha kuvutiwa na kiti cha ubunge cha Kibra kilipowachwa wazi kufuatia kifo cha Ken Okoth baada ya kuugua saratani kwa muda mrefu mnamo 2019.

Prezzo alijiunga na Wiper mwaka huo lakini baadaye akajiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho.

“Ndio nitaingia kwenye kura, Mungu akinijaalia uzima na afya njema sioni kwanini, lengo langu ni kuleta mabadiliko ambayo watu huwa wanaahidi kuleta lakini wakifika huko hawaleti. hilo."