Kifo cha babangu kilifanya nisiwahi kusherehekea Valentine's- Hamisa Mobetto afunguka

Muhtasari

•Mobetto amefichua kwamba kwa miaka mingi hakuwa anasherehekea siku ya wapendanao kama watu wengine.

Image: INSTAGRAM// HAMISA MOBETTO

Aliyekuwa mpenzi wa Diamond Platnumz, Hamisa Mobetto amefunguka kuhusu jinsi amekuwa akiadhimisha siku ya Valentine's.

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Mobetto amefichua kwamba kwa miaka mingi hakuwa anasherehekea siku ya wapendanao kama watu wengine.

Mobetto amesema kuwa kwa miaka mingi siku ya wapendanao ilikuwa ya huzuni kwake kwa kuwa ilimkumbusha siku ambayo alimpoteza baba yake. Alisema kuwa mpenzi wake wa zamani alimfanya aipende siku hiyo kwa kusherehekea naye.

"Kwa miaka michache ambayo imepita nimekuwa nikisherehekea Valentines na Ex wangu (enzi hizo alikuwa mpenzi). Kwa wale wanaonijua wanafahamu kuwa nilimpoteza baba yangu siku ya Valentines. Kwa hivyo sikuwaga na tabia ya kusherehekea Vday kabla yake (Ex). Alinifanya nipende Valentines" Hamisa alisema.

Mama huyo wa watoto wawili alieleza kwamba mwaka huu alikuwa na shaka iwapo angesherehekea Valentine's kwa kuwa tayari wametengana na mpenziwe ambaye alikuwa  anasherehekea naye.

Mobetto alipatwa na mshangao baada ya mpenzi huyo wake wa zamani ambaye hajatambulishwa kumwonyesha upendo kwa kumpa zawadi kochokocho.

"Alisema eti anajua siku hii huwa ngumu kwangu kwa hivyo akanipatia zawadi" Alisema Mobetto.

Mobetto hata hivyo aliweka wazi kwamba haimaanishi wamerudiana naye huku akimtakia heri katika mahusiano yake mapya.

"Hapana, hatujarudiana. Ni vile tu ukiwa mtu mzuri watu hukukumbuka" Mobetto alisema.

Kati ya zawadi ambazo Mobetto alipokea kutoka kwa mpenzi huyo wake wa zamani maua pamoja na pesa.