Wasanii Tanzania walalamikia tozo kubwa ya kufanya muziki

Muhtasari

• Muongozaji wa video maarufu nchini Tanzania, Hanscana amelalamikia kiwango kikubwa cha pesa ambazo wanatozwa kabla ya kufanya video za ngoma.

• Mbosso pia amelalamika kwamba licha ya kufanya video za ngoma zake zote kwenye vivutio lakini alinyimwa ubalozi.

Mbosso, Hanscana, Lavalava
Image: Instagram

Muongozaji wa video maarufu nchini Tanzania, Hanscana amelalamikia kiwango kikubwa cha pesa ambazo wanatozwa kabla ya kufanya video za ngoma kwenye maeneo mbalimbali kama vivutio vya kitaifa.

Akiandika kwenye ukurasa wake wa Instagram, Hanscana aliteta sana na kusema kwamba tozo hiyo kubwa huwabana sana na kuwapelekea wasanii kufanya video zao kwenye mazingira yasiyoridhisha kwa kushindwa kulipia maeneo ya kifahari kwa ajili ya video shoot.

“Moja ya changamoto tunayopitia kwenye kushoot nchini ni TOZO nyingi mmmno tunapohitaji kushoot kwenye VIVUTIO VYA UTALII vya Taifa (NATIONAL PARK). Wakati tukishoot hapo ni moja ya sehem kubwa ya kutangaza vivutio vyetu,” alilalama Hanscana.

Pia ameteta kwamba sehemu zingine wanadai kiwango cha juu tena kwa malipo ya dola pekee kwani hawataki kupokea shilingi za Kitanzania na pia wanahitajika kuandika barua, jambo ambalo amelipinga na kusema kwamba inafaa waruhusiwe kuchukua video kwenye vivutio vya kitalii kwani kwa kufanya hivyo pia ni njia moja ya kuitangaza nchi na vivutio vyake kwa watalii wa kigeni.

“Tulivohitaji kushoot kwenye magofu ya kale uongozi wa pale walihitaji hela nyingi mmno tena kwa DOLLER sio TSH na hawakutaka maongezi kabisa. Mpaka tukaamuwa ku cancel. Shida sio kulipia Shida ni UNALIPIA KUITANGAZA NCHI hapo ndo UZALENDO unapokosa maana. Second basi bora malipo yawe aina moja ila ukilipia hiki unaambiwa kuna kingine pia yani vipengele vingi ssssana Eg kunabaadhi ya hifadhi inabidi ulipie 1. Mtu kuingia kwenye hifadhi 5900 per person Per Day 2.gari kuingia kwenye hifadhi 70k per day 3. Kulala kwenye hifadhi yani hotel unalipa na wenye hifadhi pia unawalipa 20k per person per day 4.kushoot kibali 200k per day,” aliandika Hanscana.

Wasanii mbalimbali ambao amewahi fanya kazi nao pia wamefurika kwenye post hiyo na kudondosha hoja zao kuhusiana na hili suala ambapo wengi wameonekana kukubaliana nay eye kwa mambo kadhaa.

Msanii Mbosso amelalama pia kwamba yeye ngoma zake karibia zote amezifanyia video kwenye vivutio tofauti vya kitaifa lakini alipojaribu kuwasilisha ombi la kupewa ubalozi ili kutangaza vivutio vya nchi yake kwa watalii alinyimwa na dili hiyo ikapewa msanii mwingine ambaye hata haishi Tanzania.

“Kama wewe nimfatiriaji Mzuri Wa Kazi Zangu mbali na Zile tulizofanya Pamoja Kaka Hancana, Utaguandua Mimi ni Msanii ninayeongoza Kushoot Kwenye Mazingira Sahihi Ya kuitangaza Nchi Yangu na Sana Sana Huwa Nafanya Kwenye sehemu za Vivutio Vya Taifa. Mfano Nadekezwa - Ngorongoro Arusha, Tamu - Hifadhi Ya Taifa Kitulo (Mbeya), Hodari – Zanzibar, Ate - Ruaha National Park Iringa na Maeneo Mengi Ambayo Kwa Pamoja Siwezi Kuyaorodhesha. Lakini Sehemu Hizi zote Tulishoot Kwa Changamoto Sana. Nikaona Labda Nijaribu Kuwasilisha Hata Ombi La Kuwa Balozi Wa Utalii ili Mambo Yawe Rahisi Akapewa Msanii Flani Kutoka Nchi Flani Yani Haishi Kabisa Tanzania. Manager Wangu wa Wakati Huo alikuwa @msbrowntz Alichoka Hata Kufatilia Kwenyewe Maskini.  Tatizo Sio Kulipia Locations ila inaumiza Sana Unaenda Kushoot Mazingira Ya Nchi Yako Kuyatangaza Na Bado Unapewa Bei Za Tamaa. Inarudisha Sana Nyuma,” aliandika Mbosso.

Lavalava pia alilalama kwamba alitaka kufanya cover ya ngoma yake lakini gharama ya kushoot ikawa juu ila cha ajabu ni kwamba msanii mwingine kutoka nje ya nchi alifika hapo akapewa kibali cha kufanya video kwa gharama ya bure.

“Nilishawahi Kutaka Kupiga Picha Ya Cover Yawimbo Wangu Sehemu Fulani....Nikaambiwa Gharama Yake Ni Milioni Tano Zakitanzania Na Niandike Barua Kwanza Baada Ya Mwezi Ndoijibiwe Sasa Sijui Nikwanini Alafu Angetaka Raia Wa Nchi Nyingine Angepewa Hata Kwabure Yani Bongo Sijui Wanamatatizo Gani,” aliandika Lavalava.

Wasanii wengi tu wameonekana kutupa lawama kwa uongozi wa Sanaa nchini Tanzania huku wakiwataka wasanii ambao walioko bungeni kama meneja wa Wasafi, Babu Tale na mbunge Mwana FA kulifikisha hili bungeni ili wasanii waache kuhangaishwa kwa tozo kubwa ya kulipia sehemu za kufanya video.