Mulamwah akana madai ya kudanganya kwamba haoni mwanawe

Muhtasari

• Mchekeshaji Kendrick Mulamwah amejikuta pabaya baada ya wanamitandao kumshambulia kwa kile walisema kwamba anatoa taarifa tofauti kuhusu kuona mwanawe Keilah.

• Mulamwah amejitetea kwamba mahojiano ambamo anasikika akisema huwa anaona mtoto ni ya kitambo lakini yamepakiwa juzi.

Mulamwah
Image: Facebook

Mchekeshaji Kendrick Mulamwah amejikuta pabaya baada ya wanamitandao kumshambulia kwa kile walisema kwamba anatoa taarifa tofauti kuhusu kuona mwanawe Keilah.

Juzi katika mahojiano na mchekeshaji Dr. Ofweneke, Mulamwah alisema kwamba wako na maelewano mazuri sana na aliyekuwa mpenzi wake Carrol Sonie na kwamba huwa anaruhusiwa kuona mtoto muda wowote.

Katika mahojiano hayo, Dr Ofweneke alimuuliza kuhusu mwanawe na akasema kwamba huwa wanazungumza na mama ya mtoto wake na kwamba Sonie hajamuwekea vikwazo vyovyote kwa kuwa huwa wanashauriana na kuelewana ni vipi na lini ataona mwanawe.

Hili lilikanganya watu wengi alipotoa majibu tofauti katika Q&A kwenye Instagram yake kwamba hajawahi ona mwanawe na hata hajui kama bado mamake alimbadilisha jina au bado ni lile ambalo Mulamwah alimpa mwenyewe. Pia mchekeshaji huyo alisema kwamba Sonie alimnyoa mwanawe kinyume na tamaduni za kwao.

Wafuasi wake wamemjia juu kwenye mtandao wa Instagram kwa kile walimtuhumu kwa kutoa taarifa kinzani kuhusu kuona mwanawe lakini amejitetea na kusema kwamba mahojiano ambayo Dr. Ofweneke aliyaachia juzi yalifanyika kitambo sana wakati alikuwa bado anaona mwanawe ila kwa siku za hivi karibuni amefungiwa kabisa hawezi muona mtoto.

“Mulamwah acha kudanganya, si juzi ulisema katika mahojiano na Dr. Ofweneke kwamba huwa unaona mtoto? Unamfanya Sonie kuonekana mbaya,” shabiki mmoja alilalama.

“Hayo mahojiano yalifanyika kitambo sana. Hata nilikuwa na nywele bado. Hata kama mahojiano hayo yalipakiwa hivi majuzi lakini ni ya kitambo. Huwa sipendi kuzungumzia mambo kama hayo isipokuwa wakati imebidi,” alijitete Mulamwah.

Je, unahisi Mulamwah anadanganya ama anasema ukweli kama baba Keilah?