Nimezoea! Mulamwah azungumzia kuonewa Mitandaoni

Muhtasari

• Mchekeshaji Mulamwah amesema hababaishwi tena na watu wanaomsimanga katika mitandao ya kijamii na kwamba amezoea.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji Kendrick Mulamwah amefunguka mbinu ambazo anazitumia kushinda msongo wa mawazo ambao unasababishwa na kuonewa na kutukanwa mitandaoni yaani cyber bullying.

Akijibu maswali kutoka kwa wafuasi na mashabiki wake kwenye mtandao wa Instagram kwenye Q&A, Mulamwah amesema kwamba tangu amepata umaarufu wa mitandaoni, amepitia manyanyaso mengi kutoka kwa watu mbali mbali wakifanya mzaha kutokana na maumbile ya mwili wake na kwa sasa amezoea wala hababaishwi tena na masimango ya mitandaoni.

“Inachukua nini kuwa na ukakamavu kama huo wako, haswa ukikumbuka kwamba wewe umevutwa sana kwenye matope na kusimangwa pakubwa na waonevu wa mitandaoni” shabiki mmoja aliuliza.

“Nimezoea. Ni kawaida mpya kwangu. Siku hizi sipigani na huzuni wa kuonewa mitandaoni, nimezoea kwa sababu najua siku moja wale wanaonisimanga watachoka na kuacha kunionea kwenye mitandao,” alijibu Mulamwah.

Kwa muda mrefu watu wamekuwa wakimburuza mitandaoni kwamba hana maskio wengine wakisema ndevu zake ni mbaya na itakumbukwa wakati mmoja amekejeliwa mitandaoni mpaka akafikia hatua ya kulia kwa ghadhabu na kulivua shati lake na kisha kulichoma moto.