Muigizaji Muna Love awazia kubadili dini, aibua maoni kinzani

Muhtasari

• Muna Love awazia kubadilisha dini kutoka ukristu kwenda uislam, auliza maoni kama waislam watamchamba kama walokole au watampokea.

• Msanii Alikiba amhakikishia kumstiri pindi atakapoafikia maamuzi ya kujiunga na dini ya uislam, huku wengine wakisema ni kuchanganyikiwa.

Muna Love
Image: Instagram

Muigizaji na mfanyibiashara Muna Love ametangaza nia yake ya kubadili dini kutoka Ukristu kwenda Uislam kwa kile alichokitaja kuwa ni masimango ya mara kwa mara na wakristu walokole.

Muigizaji huyo aliandika kwenye Instagram yake wikendi iliyopita kwamba anataka kubadili dini kwa sababu amechoka na kurushiwa maneno ya kebehi na walokole wanaokosoa mitindo ya uvaaji wake na mambo anayoyafanya mitandaoni.

Akiweka kwenye mizani maamuzi hayo, aliwauliza wafuasi an mashabiki wake kutoa mawazo kuhusu nia yake hiyo kabla hajatekeleza maamuzi hayo na kuwauliza waislam kama watampokea ama watamsusa.

“Hivi nikiamua kubadili dini kuwa muislam, Waislam watanipokea au nao wanaweza kunichamba kama hawa walokole? Nikafa,” aliuliza Muna Love kwenye Instagram.

Watu mbalimbali walifurika kwenye upande wa kuandika maoni na waislam wakamhakikishia kumpokea katika dini huku walokole wakimsuta na baadhi wakimtaka awape nguo zake zinazoonesha maungo ya mwili pindi atakapojiunga na Uislam kwani dini hiyo huwa haikubali watu kuvaa nguo kama hizo.

Ila kilichowasisimua wengi ni maoni ya msanii wa bongi fleva, Alikiba ambaye pia alikuwa miongoni mwa watoa maoni ambapo alimwambia Muna Love kwamba atahakikisha amestirika pindi atakapoafikia maamuzi ya kuwa muislam.

“Uislam ni dini uliyozaliwa nayo ila unapofanyiwa ubatizo ndio unakuwa converted into Christian. Mimi nitahakikisha unastirika. I hope unakumbuka maneno yangu, na iwe kheri ALLAH akufanyie wepesi dada yangu,” aliandika Alikiba.

wengine walimtaka kubaki katika ukristu huku wakisema kwamba huenda amechanganyikiwa na ni vizuri kama angechukua likizo kutoka mitandaoni ilikutuliza akili yake na asikurupukie maamuzi ambayo huenda akayajutia siku za mbeleni.

"Njia Ya Wokovu Ina Mambo Mengi; Ila Kaa Ndani Ya Yesu Naumpende Bwana na Moyo Wako wote! This Too Shall Pass," aliandika aliyekuwa msanii wa injili kutoka Kenya, Bahati.

"Ningekushauri uchukue mapumziko kidogo kwenye mitandao ya jamii,afya ya akili ni jambo la msingi sana,nakuona kabisa hauko sawa," mwingine alitoa ushauri.

Muigizaji huyo amekuwa akiibua maoni kinzani, huku akionekana kuchanganyikiwa kabisa tangu afiwe na mtoto na baadhi wanahisi hicho ndicho kitu kinachomkosesha amani ya akili.