Diamond, Rayvanny waongoza kwenye chati za kutazamwa sana YouTube

Muhtasari

• Wasanii wa lebo ya Wasafi wazidi kung'ara kwenye mtandao wa YouTube huku Nandy na Alikiba wakiporomoka.

Diamond, Rayvanny, Zuchu, Harmonize

Msanii Diamond anazidi kudedea katika chati za muziki ambako ameongoza katika orodha ya wasanii wa Tanzania waliotazamwa sana kwenye mtandao wa YouTube kwa mwezi Februari pekee.

Katika orodha hiyo iliyotolea Jumanne na Chart Data Tz, wasanii wa rekodi lebo ya Wasafi wanazidi kuongoza kwa kutazamwa sana kwenye mtandao wa YouTube huku Harmonize ambaye pia wakati mmoja alikuwa mwanafamilia wa Wasafi akiwafuatia kwa ukaribu mno naye Alikiba akizidi kuporomoka zaidi huku wanamuziki wapya kwenye game wakimpiku katika kutazamwa YouTube.

Orodha hiyo inaonesha kwamba msanii Diamond Platnumz alitazamwa Zaidi kwenye YouTube na watu milioni 35.3, akifuatiwa na Rayvanny kwa watu milioni 18.9, Zuchu watu milioni 18.6 naye Harmonize akifunga nne bora na watu milioni 16 ambaye ndiye wa mwisho katika orodha hiyo kuwa na watazamaji Zaidi ya milioni 10 kwenda mbele.

Baadhi ya mambo ambayo yalionekana wazi vilevile ni chati za wasanii kama vile Alikiba na Nandy ambao kwa mwezi wa Februari hawajafanya vizuri sana katika mtandano wa YouTube ambako kazi za Alikiba zilifuatiliwa na watu milioni 7.1 pekee huku Nandy akiwa amefunga kumi bora na watu milioni 2.43 pekee.

Msanii MacVoice amewashangaza wengi baada ya kutazamwa na watu milioni 2.51 na kumpiku Nandy kwa kushikilia nafasi ya tisa. Ikumbukwe msanii huyu ni miongoni mwa wasanii wapya kabisa kwenye tasnia ya muziki wa bongo na ambaye atoa ngoma zake chini ya rekodi lebo mpya ya msanii Rayvanny, Next Level Music.

Image: Instagram