Eric Omondi anasema Young Famous & African iliiba mawazo ya Wife Material

Muhtasari

• Mfumo uliotumika katika Young Famous and African ni mfumo sawa na ule wa Wife Material. Kuna mtu alikuwa akitazama chini ya maji na kuiba mawazo yetu - Eric Omondi

Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mchekeshaji Eric Omondi sasa anadai kwamba mfumo unaotumika katika kipindi ambacho kinaendelea katika mtandao wa Netflix, maarufu kama Young, Famous and African huenda uliibwa kutoka kwa kipindi chake cha Wife Material.

Omondi aliandika kupitia instastories zake akisema kwamba baada ya kutazama kipindi hicho cha Netflix ambacho kinawahusisha watu maarufu kutoka bara la Afrika, hatimaye ameafiki kwamba hakuna tofauti na kile alichokuwa akifanya kwenye Wife Material yake.

Anasema labda kuna mtu alikuwa anavizia Wife Material chini ya maji na kuiba mawazo na mtiririko wake na baadae wakaunda hiyo ya Young African and Famous ambayo kwa sasa ni gumzo kubwa mitandaoni.

“Mfumo uliotumika katika Young Famous and African ni mfumo sawa na ule wa Wife Material. Ni aidha kuna mtu alikuwa akitazama chini ya maji na kuiba mawazo yetu au ni mawazo tu yaligongana vizuri kweli yaani,” aliandika Eric Omondi.

Mjadala huu unakuja siku mbili tu baada ya baadhi ya Wakenya kuhisi kwamba Wakenya maarufu wangeshirikishwa katika kipindi hicho cha uhalisia kinachoruka kupitia Netflix.

Afrika mashariki imewakilishwa na msanii Diamond kutoka Tanzania na aliyekuwa mpenzi wake Zari kutokea Uganda.