Babalevo afurahia BASATA kumsimamisha kazi Steve Nyerere

Muhtasari

• Babalevo alionyesha furaha yake baada ya BASATA kumsimamisha kazi Steve Nyerere kama msemaji wa wanamuziki.

• Alishikilia kwamba Nyerere alikuwa anawagawanya wasanii kwenye makundi.

Instagram, KWA HISANI
Instagram, KWA HISANI
Image: Babalevo

Msanii na mwanahabari kutoka Tanzania, Babalevo ameonyesha furaha yake baada ya BASATA kumsimamisha kazi Steve Nyerere kama msemaji wa wanamuziki.

Akizungumza katika mahojiano na wanahabari, Babalevo alisema kwamba Nyerere alikuwa anawagawanya wasanii katika makundi ya wale wanaokubali uongozi wa serikali ya rais Samia Suluhu na wale wanaoikosoa serikali hiyo.

Kulingana na Babalevo, 'utimu' huo ulikuwa unaharibu gemu la burudani nchini humo.

Alisema kwamba Nyerere alipaswa kupigana ili kuwaunganisha wasanii ili kuhakikisha miziki yao inafika ulimwenguni kote.

"...Mimi leo serikali kupitia BASATA imenifurahisha sana kwa kumpiga stop Steve Nyerere,"

Alisema kwamba iwapo Nyerer ataendelea kushikilia wadhfa huo wa usemaji, basi wanamuziki wote wa nyimbo za bongo watajiondoa katika shirikisho hilo.

Babalevo alishikilia kwamba viongozi waliopo bungeni ambao pia ni wasanii ndo pekee wanaoweza kuhakikisha matakwa yao yanaafikiwa.

Kwa upande wake Nyerere alisema kwamba, kitendo cha wasanii kupinga uteuzi wake ni sehemu ya kazi na hivyo hawezi kusumbuliwa na jambo hilo.

Kwa sasa wasanii na mashabiki watazidi kusubiria kujua hatma ya Nyerere iwapo atazidi kusalia ofisini ama atabanduliwa na nafasi yake kuchukuliwa na mtu mwengine.