Harmonize amvulia kofia Eric Omondi, amtambua kama mchekeshaji mkubwa zaidi Afrika Mashariki

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo alimtambulisha Eric kama nduguye mkubwa na mchekeshaji mkubwa zaidi Afrika Mashariki.

•Eric ambaye alitimiza miaka 40 hivi majuzi amekuwa akijipiga kifua kuwa miongoni mwa wachekeshaji bora bara Afrika na kote Duniani.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE, ERIC OMONDI

Mchekeshaji mashuhuri aliyezingirwa na drama nyingi, Eric Omondi kwa sasa yupo nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi.

Eric alitua katika nchi hiyo jirani siku ya Jumatatu na kupokewa na staa wa muziki wa Bongo, Harmonize.

Katika kanda ya video iliyopakiwa na Harmonize, wasanii hao wawili walioneka wakibarizi na kucheza mpira wa vikapu nyumbani kwa mmiliki huyo wa lebo ya Konde Gang. Mwanamuziki huyo alimtambulisha Eric kama nduguye mkubwa na mchekeshaji mkubwa zaidi Afrika Mashariki.

"Kaka yangu Eric Omondi, mchekeshaji mkubwa Afrika Mashariki alifika kijijini," Harmonize alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Eric ambaye alitimiza miaka 40 hivi majuzi amekuwa akijipiga kifua kuwa miongoni mwa wachekeshaji bora bara Afrika na kote Duniani.

Siku za hivi majuzi amejikita katika mstari wa mbele kupigania muziki wa Kenya huku akitaka uchezwe na ukubalike zaidi.