Harmonize asitisha kutoa muziki siku chache baada ya kumlilia Kajala amrudie

Muhtasari

•Harmonize aliandamana na binti yake Zuuh Konde kushiriki kipindi cha mwisho studioni usiku wa Jumanne. 

•Hivi majuzi mwanamuziki huyo alitundika picha ya Kajala kwenye chumba chake cha kulala na kumsihi mwigizaji huyo arudi.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ametangaza hatatoa muziki wowote mpya katika kipindi cha takriban miezi miwili kijacho.

Bosi huyo wa Konde Music Worldwide aliandamana na binti yake Zuuh Konde kushiriki kipindi cha mwisho studioni usiku wa Jumanne. 

Kulingana na tangazo lake, Harmonize hatatembelea studio kutoa muziki mpya hadi  ifikapo mwezi Juni.

"Hakuna muziki mpya wa Konde Biy hadi Juni. Furahu Albamu kubwa  zaidi kwa bio yangu yangu," Harmonize alitangaza kupitia Instagram.

Tangazo la Harmonize linakuja siku chache tu baada yake kuonekana akijaribu kwa udi na uvumba kumbembeleza aliyekuwa mpenziwe Kajala Masanja kumrudia.

Hivi majuzi mwanamuziki huyo alitundika picha ya Kajala kwenye chumba chake cha kulala na kumsihi mwigizaji huyo arudi.

"Wewe ndiye mtu pekee nitaona nikifungua macho yangu kila siku. Tafadhali rudi. Tabasamu kwa ajili yangu popote ulipo!!" Harmonize alimwandikia Kajala kupitia Instagram.

Hata hivyo haijulikani kama hali yake ya kumpeza Kajala imechangia kwa namna yoyote katika hatua ya kusitisha muziki.

Katika kipindi hicho cha miezi miwili, mwanamuziki huyo amepanga kutumbuiza katika mataifa matano tofauti.

Harmonize atatumbuiza jijini Nairobi na Mombasa mwezi Aprili. Mwezi Mei atatumbuiza nchini Burundi na  jijini Dar Es Salaam. Juni atafanya ziara ya muziki nchini Uganda, Rwanda na jijini London.