"Sijui mbona mnasema Pritty Vishy si mrembo, ama ni vile hatumii filters? - Madini Classic

Classic wikendi iliyopita alisema yuko tayari kutoa mahari milioni 4 ili kumuoa Vishy

Muhtasari

• "Ni kwa sababu hajui kudeka na kutumia simu zenye picha za urembo kupakia mitandaoni kama baadhi yenu?" - Madini Classic

Msanii Madini Classic na mchumba wake Pritty Vishy katika hafla moja awali
Msanii Madini Classic na mchumba wake Pritty Vishy katika hafla moja awali
Image: Instagram

Mwanamuziki anayedai kuwa ndiye mpenzi mpya wa mkuza maudhui na mwanafasheni Pritty Vishy, Madini Classic amewasuta wale wanaosema kwamba mwanadada huyo si mrembo na kusema kwamba kwa macho yake Vishy ndicho kitu kizuri zaidi alichowahi kukipata katika maishac yake.

Akipakia picha ya mazungumzo ya WhatsApp ambayo mtu mmoja alikuwa anataka kujua kama ukaribu wake kama mpenzi na Pritty Vishy ni mapenzi ya ukweli ama ni kiki, Madini Classic alimjibu kwamba ni mahusiano ya kimapenzi kweli na ameamua kumuoa.

“Kwa hiyo uliamua kumuoa wewe hata si ungekuja unioe mimi ama hutaki kuzaliwa watoto wazuri,” shabiki huyo alimuuliza.

Madini alicharuka na maneno haya ambayo kwake yaligonga kama kashfa na kumtaka shabiki huyo kukoma kwani Vishy ni mrembo na atamzalia watoto wazuri pia kama mwanamke yeyote mwenye urembo wake wa kiasili.

“Sielewi ni kwa nini wengi wenu mnadhani Pritty Vishy si mrembo. Ni kwa sababu hajui kudeka na kutumia simu zenye picha za urembo kupakia mitandaoni kama baadhi yenu? Mnafaa kukutana na hilo toto moja kwa moja na ndio mtakubaliana na mimi kwamba yeye ni mrembo kupita maelezo,” aliandika Madini Classic kwenye Instagram yake.

Pritty Vishy alifurahikia utetezi huu wa Madini Classic ambaye sasa anasema ni mchumba wake, licha ya wengi kubaki kwenye mataa wasijue kama kweli ni kiki ama ni uchumba wa ukweli.

“Waambie mpenzi,” Vishy aliandika.

Vishy na mpenzi wake wa zamani Stevo Simple Boy waliachana miezi michache iliyopita ambapo walichafuana ya nguoni kweney mitandao ya kijamii na mpaka sasa kila mmoja amekuwa akicheza safu yake ifaavyo kumuonesha mwingine kwamba kweli ameshajipa shughuli kimaisha na kupata unafuu kuliko awali wakiwa pamoja.

Pritty Vishy alitangaza kwamba mahari yake ni shilingi milioni 2 pesa za benki kuu ya Kenya na wikendi iliyopita msanii Madini Classic alisema kwamba kwa urembo ule basi yuko radhi hata kutoa milioni 4 kama mahari ilmradi tu apate kuwa na lepe la usingizi kando ya Vishy katika maisha yake yote.