"Babe siko sawa, nahitaji penzi!" Jimal Rohosafi amsihi mkewe Amira

Jimal alisema huenda ni kutokana na kupost kwake kwingi kunamfanya Amira kudhani ako sawa ilhali anahitaji penzi

Muhtasari

• Jimal kwa wiki kadhaa sasa ameonekana akijutia vitendo vyake dhidi ya Amira na kuomba msamaha hadharani.

Mfanyabiashara Jimal Rohosafi
Mfanyabiashara Jimal Rohosafi
Image: Instagram//JimalRohosafi

Mfanyibiashara Jimal Rohosafi kwa mara nyingine tena baada ya kuruhusiwa kuondoka hospitalini baada ya kusemekana kulazwa ameendelea kumbembeleza mpenzi wake ambaye ni mzazi mwenziwe, Amira kumrudia.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Jimal Rohosafi aliachia ujumbe wa moja kwa moja safari hii bila kupitia vichochoroni kwa kumwambia mpenzi wake kwamba anataka mapenzi yake japo kidogo tu.

Jimal alisema kwamba pengine ni kutokana na hali yake ya kupakia kila mara mitandaoni ndio inamfanya Amira kudhani kwamba yuko sawa lakini kutoka moyoni ukweli ni kwamba anaumia na anahitaji kukandwa na kupetiwa peti kaam mpira wa kitenesi.

“Shida yangu ni kwamba ninapost sana na mahabuba wa moyo wangu anafikiri niko sawa. Mpenzi wangu nahitaji mapenzi,” Jimal Rohosafi alifunguka wazi sasa liwalo na liwe.

Mfanyibiashara huyo ambaye ukwasi wake mkubwa ni kutokana na biashara katika sekta ya matatu na kuwa na karakana ya kupamba matatu za jijini Nairobi amekuwa kwa muda wa takribani mwezi mmoja sasa akimbembeleza mke wake Amira kumrudiana na mpaka kwa wakati mmoja alionekana kujutia vitendo vyake vya awali vilivyosambaratisha ndoa yao ya miaka mingi.

Jimal aliachwa na Amira mwishoni mwa mwaka jana katika kile kilichoonekana kama ni wivu wa mapenzi baada ya Jimal kutoka kimapenzi na mwanamitindo Amber Ray na mpaka kumfanya mke wa pili.

Hili lilimghadhabisha Amira aliyefungasha virago vyake na kuondoka zake na miezi michache baadae, Amber Ray naye alimshiba Jimal na kumtema pia, kumuacha amebaki jangwani pasi na mtu wa kumkimbilia kwa kumbato.