Vera Sidika wa Ukambani, nataka kuongeza makalio - Justina Syokau

Mwanamuziki huyo anataka kupunguza mafuta ya mwili wake ili yawekwe kwenye makalio

Muhtasari

• Mwanamuziki huyo aliongeza kuwa amejaribu mbinu tofauti ili kupunguza mwili wake bila kufanikiwa kuupunguza.

• Syokau aliongeza kuwa ingawa amebarikiwa kuwa na makalio makubwa asili bado anataka kufanyiwa upasuaji wa kuongeza makalio na kupunguza tumbo.

Justina Syokau

Mwanamuziki Justina Syokau amefichua kuwa anataka kufanyiwa mchakato wa liposuction wa kupunguza mwili wake.

Syokau alisema kuwa hana shida na mchakato huo kwani utautengeneza mwili wake kuwa anavyotaka yeye.

Aliongeza kuwa mwili wake ni hekalu ya Yesu ambao unahitaji kutunzwa kulingana na mafunzo ya Bibilia.

Mwanamuziki huyo alisema kuwa amejaribu mbinu tofauti ili kupunguza mwili wake bila kufanikiwa kuupunguza.

"Nataka kutengeneza mwili wangu, hata natafuta milioni 3. Yaani si ukiumwa na jino huwa unaenda hospitalini kung'olewa jino hilo? Sasa mimi nataka kutolewa mafuta kwenye mwili wangu ili yawekwe mahali inayostahili, kwa utukufu wa Mungu," Justina alieleza sababu yake.

Alisema kuwa tumbo chake kinamsumbua na kuwa anataka kuyatoa mafuta ambayo yako kwenye mwili wake ili ukae zuri.

Syokau aliongeza kuwa ingawa amebarikiwa kuwa na makalio makubwa ya  kiasili bado anataka kufanyiwa upasuaji wa kuongeza makalio na kupunguza tumbo.

Mwanamuziki huyo alisema kuwa amejaribu kufanya mazoezi na hata kupunguza chakula anachokula ili kupunguza mwili wake ila bado haupungui.

Aliongeza kuwa hata watu wakikemea mchakato huo bado wanataka kufanyiwa liposuction ila kisisrisiri.

"Nataka kutoa mafuta kwa tumbo, kwa mapaja na kwa mgongo ili yote yapelekwe mahali pamoja ambapo ni makalio. Watu wanasema kuwa hawataki lile umbo la Vera ila mimi nalitaka, lile umbo ni zuri, bora ulitumie kwa utukufu wa Mungu," Syokau alisema huku akieleza anavyotaka umbo lake liwe.

Aliongeza kuwa yeye huvaa mshipi wa kubana tumbo na huwa hapendi hali hiyo ya kutokuwa kwenye starehe.

Baadhi ya wanawake maarufu ambao wamefanyiwa mchakato huo wa liposuction ni mwanablogu wa YouTube Murugi Munyi, waigizaji Jackie Matubia na Kate Actress mwanasosholaiti Risper Faith miongoni mwa wengine.

Hivi majuzi mwanasosholaiti  wa Nigeria, Amelia Pounds alifariki akifanyiwa upasuaji huo wa liposuction huko India.