Diamond aifuta video akiwadanganya Tiffah na Nillan kuwa ndio wanawe wa pekee

Diamond alionekana akiwaaminisha wanawe hao kuwa hana watoto wengine kando nao na siku mbili baadae aliifuta.

Muhtasari

• Watu walimkashfu kwa kitendo hicho cha kuwahadaa watoto na kumtaka kuwaambia ukweli.

Diamond na familia yake na Zari
Diamond na familia yake na Zari
Image: Maktaba

Msanii Diamond hatimaye ameifuta video aliyoipakia kwenye Instagram yake ikimuonesha na familia yake na Zari.

Katika video hiyo yenye utata, Diamond alionekana akiwaambia watoto wake Tiffah na Nillan kwamba hana watoto wengine kando nao, kitu ambacho kiliibua ukakasi mkubwa kutoka kwa baadhi ya mashabiki wake lakini pia dadake na mamake pia.

Wengi walimsuta Diamond kwa kuwadanganya watoto wake kuwa hawana ndugu wengine kando na wao na kumtaka kuwaambia watoto ukweli ili wakue wakijua kuna ndugu zao kando na wao na hata kukutanishwa ili kujenga ukaribu wa kifamilia mapema wanapokua.

Umewakosea watoto ulitakiwa uwaambie kuna Tom kaka pia ndugu yao ili wajenge mapenzi tangu wakiwa wadogo kama vipi wakutane nae pia,” Esma alionesha kutoridhishwa kwake na hatua ya Diamond kukataa mbele ya watoto wake kuwa ana watoto wengine nje.

Mama yake pia alionesha kuchukizwa na maelezo ya Diamond kwa wanawe kuwa hana wengine nje ya ndoa. Ikumbukwe Mama Dangote kwa muda mrefu amekuwa akidhihirisha mapenzi yake kwa mtoto wa Diamond na Tanasha Donna kutoka Kenya, Naseeb Junior.

Baada ya masimango haya kumkaba kwenye koo, msanii huyo sasa ameifutilia mbali video ile ila hajatoa maelezo yoyote. Inasubiriwa kama msanii huyo atajitokeza wazi kutetea hatua yake ya kuwahadaa wanawe au pia kuzungumzia kiini cha kuifuta video ile ambayo mpaka kufutwa kwake ilikuwa imejizolea watazamaji laki mbili na nusu.