'Made For Us' ndio albamu yangu ya mwisho katika lugha ya Kiswahili - Harmonize

Msanii huyo alijisifia kwamba hakuna msanii katika kizazi hiki ambaye amefanikiwa kutoa albamu kwa miaka mitatu mtawalia.

Muhtasari

• 2020 Afro East, 2021 Highschool, 2022 Made For Us. Hakuna msanii mwingine ambaye amefanikiwa kufanya hivi katika kizazi hiki - Harmonize.

HARMONIZE
HARMONIZE
Image: INSTAGRAM

Mkurugenzi mkuu katika lebo ya Konde Music Worldwide ambaye pia ni msanii, Harmonzie amedokeza kwamba albamu yake ya hivi punde, Made For Us huenda ikawa ndio yake ya mwisho kufanya nyimbo kwa lugha ya Kiswahili.

Msanii huyo alidokeza haya kupitia Instagram Stories zake, siku mbili tu baada ya kuzindua albamu hiyo yenye ngoma zaidi ya kumi na nne.

Harmonize pia alijivika koja la maua kwac kusema kwamba katika kizazi chake, hakuna msanii mwingine ambaye amefanikiwa kutoa albamu kila mwaka kwa miaka mitatu mtawalia na zote zenye ngoma zenye mnato ajabu.

“Miaka mitatu, albamu 3 zenye uzito wa aina yake. 2020 Afro East, 2021 Highschool, 2022 Made For Us. Hakuna msanii mwingine ambaye amefanikiwa kufanya hivi katika kizazi hiki. Pengine Made For Us ndio albamu yangu ya mwisho ya Kiswahili,” Harmonize alidokeza.

Pia aliwaahidi mashabiki wake kwamba Ijumaa hii ana jambo lake kubwa ambalo atawadokezea na kuwataka kukaa mkao wa kula wakisubiria tangazo lake kubwa mwishoni mwa juma.

Hivi majuzi msanii Otile Brown kutoka Kenya baada ya kurejea kutoka ziara yake ya muziki nchini Marekani alizunumzia kizingiti kikubwa katika muziki wa Afrika Mashariki akisema kwamba lugha ya Kiswahili inaubama muziki wa ukanda huu kutotusua katika masoko ya kimataifa.

Kwa kudokeza kwamba huenda albamu ya mwaka huu itakuwa yake ya mwisho kufanya katika lugha ya Kiswahili, msanii huyo anaweka malengo yake wazi kwamba anataka kuteka tasnia ya muziki nje ya ukanda wa Afrika Mashariki kwa kushindana na wasanii wakubwa kimataifa.

Ikumbukwe wiki jana alidokeza kwamab yumo mbuioni kuidai nafasi ya kwanza katika orodha ya wasanii wakubwa Afrika nzima, huku akisema kwamba nafasi hiyo ambayo kwa sasa inashikiliwa na swahiba wake wa muda mrefu, Burna Boy ataichukua hivi karibuni.

Kila la kheri Tembo!