Jinsi Harmonize alivyotumia weledi wake kimuziki kumrushia cheche kali Diamond Platnumz

Harmonize katika wimbo wake wa My Way alieleza kwa mapana mambo amabyo wengi wamekuwa wakijiuliza kuhusu kuzorota kwa urafiki wake na Diamond

Muhtasari

• Harmonize anawakomesha wenye midomo na kuwataka wamuache aishi maisha yake jinsi anavyotaka mwenyewe.

Diamond na Harmonize
Diamond na Harmonize
Image: Screengrabs: YouTube

Hatimaye msanii Harmonize mwishoni mwa wiki jana aliachia albamu yake ya tatu kwa jina Made For Us, mkusanyiko wa nyimbo 14.

Katika albamu hiyo, wimbo wa pili ambao ni ‘My Way’ umekuwa gumzo kubwa sana kwenye mitandao ya kijamii huku washikadau katika tasnia ya muziki wakiuchambua kila mmoja kwa njia yake.

Katika wimbo huo ambao umefananishwa na ule wa ‘Nawaza’ kutoka kwa EP ya FOA yake msanii Harmonize, katika mtiririko wa kujieleza, Harmonize anachukua nafasi hiyo na kueleza maisha yake huku akizungumzia mapenzi yake na wapenzi wa awali kama ambavyo yalikwenda.

Kando na kujieleza vizuri, wengi wamemsifia msanii huo kwa weledi wake katika kulainisha vina vya kati na vya mwisho katika mishororo ili kuleta ladha ya ushairi.

Humo ndani haswa haswa katika vesi ya pili, amezungumzia pakubwa maisha yake namna ambavyo anataka kuishia kwa njia yake pasi na mtu yeyote kumratibia mambo yake na ameonekana kutupa bomu kwenye himaya ya simba – Diamond Platnumz.

Harmonize kwa maneno yake anasikika akiimba kwamba hata hakutaka kuzua vita vya kimaneno na aliyekuwa babake katika muziki Diamond Platnumz ila kwamba Diamond aliingiwa na shinikizo tu la kuhofia Harmonize kumpita kimuziki.

“Hata huyo ndugu yenu mimi sikutaka vita, mbona sikugombana na Madam Ritha, ni presha tu kuhofia nampita, akisikia (kitambulisho cha kukohoa kwake) karoho kanampita,” Harmonize alimchokoza Diamond.

Itakumbukwa pia katika wimbo wake wa ‘Nawaza’ Diamond alizungumzia kwa mapana kuhusu ukakasi uliopo baina yake na msanii Alikiba huku akitaja kuwa ni ujana tu wa kugombania mashabiki ndicho chanzo cha wawili hao kutoonana jicho kwa jicho.