Kwa nini Ommy Dimpoz hana tattoo, hanywi pombe, havuti sigara wala kutoboa maskio?

Msanii huyo ni tofauti na wengine ambao wanaona kuwa na hivyo vyote ndio fasheni ya muziki wa kizazi kipya.

Muhtasari

• Ni wiki moja iliyopita ambapo msanii Diamond Platnumz alionekana akitobolewa pua na kuwekewa kipini cha puani alipozuru taifa la Malawi kwa tamasha lake la kimuziki.

Ommy Dimpoz
Ommy Dimpoz
Image: Ommy Dimpoz

Msanii Ommy Dimpoz ambaye Ijumaa alikuwa na mkutano wa wanahabari akiwataarifu kuhusu utayarifu wa kuachia albamu yake ambayo tayari ngoma zote 15 zipo kwenye majukwaa yote ya kupakua miziki aliweka wazi kwamba yeye si mraibu wa kilevi chochote.

Msanii huyo ambaye alikuwa anajibu swali ya mmoja wa wanahabari aliyetaka kubaini iwapo ametoboa maskio, haswa baada ya kuonekana amevalia herein ya maskioni, alisema kwamba wala hajatoboa maskio yake.

Alisema kuwa yale ni mapambo tu ambayo alikuwa amebandika kwenye masikio na wala hakuwa ametoboa hivyo zile herein zilikuwa za kimchongo tu na wala si za kweli zile za kuingizwa kwenye shimo ya masikioni.

Alizidi kueleza kwamba hata mwilini mwake hana mchoro wa tattoo wa aina yoyote na wala hatumii kilevi cha aina yoyote ile unachoweza kufikiria katika ardhi hii ya Mungu.

“Sijatoboa, sina tattoo, sinywi pombe wala sivuti sigara,” Ommy Dimpoz alisema huku akiweka ucheshi wake kama wengi wanavyomzoea.

Bila shaka kwa msanii mkubwa kama huyo kubainisha wazi kuwa hana tattoo na wala hajatoboa hata sehemu moja ya mwili wake kunamfanya kidogo kuwa tofauti na wenzake ambao wanakumbatia fasheni zinazoletwa na wasanii haswa kutoka nchi za ughaibuni kama kutoboa maskio na pua, kuchorwa tattoo, kusuka rasta miongoni mwa staili zingine za kimchongo.

Ni wiki moja iliyopita ambapo msanii Diamond Platnumz alionekana akitobolewa pua na kuwekewa kipini cha puani alipozuru taifa la Malawi kwa tamasha lake la kimuziki.

Kando na kutobolewa pua, Diamond pia ameiga baadhi ya mambo mengi kutoka kwa wasanii wakubwa wa ughaibuni kama kusuka mtindo wa rasta, kuvalia maguo ya kumpwerepweta lakini pia na kulimbikiza michoro kadhaa katika mwili wake.

Si Diamond tu bali pia msanii Harmonize ambaye alikiri wazi kuwa huvuta sana sigara na bangi ametoboa pua, maskio pamoja pia na kuchorwa tattoo nyingi tu, ya hivi punde ikiwa ni ya herufi ya jina la mpenzi wake Kajala kwenye kidole.