Itakuchukua muda kusahau - Harmonize amwambia Kajala baada ya kumtema

Awali Kajala alikuwa amedhibitisha kuvunja uhusiano wake na Harmonize pasi na kutaja sababu.

Muhtasari

• Hakika nimekosea familia yangu, ndugu zangu, na marafiki zangu. Kutenda kosa si kosa, kosa kurudia kosa - Kajala alisema.

Harmonize abwagwa na Kajala
Harmonize abwagwa na Kajala
Image: Instagram

Msanii Harmonize amefunguka baada ya aliyekuwa mpenzi wake Kajala Masanja kuweka wazi kuwa mapenzi yao yamefikia mwisho wa reli.

Hili linakuja siku kadhaa baada ya watu mitandaoni kuzua maswali mengi kuliko majibu kuhusu uhusiano wao, haswa baada ya kupunguza kasi ya kuonekana pamoja.Pia wawili hao walibadilisha maelezo ya bio yao mitandaoni ambapo Harmonize alikuwa anajiita mume wa Kajala naye Kajala akijitambulisha kama mke wa Harmonize.

Wote walibadilisha maelezo hayo hatua iliyozidisha uvumi kuwa huenda hawako pamoja tena licha ya kuvishana pete za uchumba mwezi Juni mwaka huu.

Kajala alikuwa wa kwanza kutema nyongo na kueleza kwa mapana kuwa hakuwa anajua alichokuwa akifanya ila akamalizia kwa kuomba radhi kwa ndugu jamaa na marafiki na pia kumsamehe mpenzi wake Harmonize.

Mimi kama mwanamke na binadamu nimeumbwa kupenda na kusamehe pia,ila kwenye hili nastahili kuchekwa, nastahili kubezwa na kudharauliwa pia😌. Sipo hapa kujitetea wala kutia huruma ni kweli nilifanya makosa na nimeyagundua makosa yangu, mimi siyo mkamilifu. Hakika nimekosea familia yangu, ndugu zangu, na marafiki zangu. Kutenda kosa si kosa, kosa kurudia kosa. Ninamsamehe EX wangu na niko tayari kwa yajayo,” Kajala aliandika.

Kupitia instastory yake, Harmonize aliandika ujumbe mfupi ulioonekana kumlenga Kajala na maneno yake ya kuvunja uchumba akisema kuwa itamchukua muda mrefu sana kusahau nyakati nzuri ambazo walikuwa wanafurahia pamoja kwa muda wote ambao wamekuwa wakichumbiana.

“Itakuchukua muda sana kuisahau,” Harmonize aliandika.

Japo wengi walishindwa kuelewa ujumbe huu mara moja, baadhi walielezea kuwa ni shoo yake alikuwa akipigia debe huku wengine wakisema ni ujumbe uliomlenga Kajala baada ya kumbwaga.