Willis Raburu afurahia kukutana na wanawe akirudi kutoka Qatar

Muhtasari

• Raburu amekuwa Qatar kwa zaidi ya wiki moja ambapo walisafiri na mtangazaji mwenza kushuhudia kombe la dunia.

Raburu na wanawe
Raburu na wanawe
Image: Facebook

Mwanahabari wa 10over10 katika runinga ya Citizen Willis Raburu amefurahia kurejea nchini kutoka Qatar na kujumuika na familia yake.

Raburu alipakia picha akiwa amewapakata wanawe wawili mikononi mwake na kusindikiza picha hiyo kwa ujumbe mfupi wa kuonesha furaha na shukrani zake kwa Mungu.

“Nahisi mzima kurejea, Neema ya Mungu,” Raburu aliandika kwenye picha hiyo.

Kituo hicho cha Runinga kilikuwa kimefadhili safari ya Raburu na mwenzake Shatta Boy kuelekea Qatar kushuhudia kipute cha kombe la dunia kutokana na mapenzi na weledi wao katika Sanaa ya spoti.

Akiwa Qatar, mkewe, Ivy Namu alidokeza kwa wanamitandao kuwa shughuli ya kuwa mlezi wa watoto wawili ilikuwa ngumu kwake na kuwa ni ya kuchosha mno hata kumkosesha muda wa kujumuika na mashabiki wake kwenye mitandao ya kijamii.

“Kwa wiki kadhaa zilizopita nimekuwa nikijihisi kulemewa kabisa kutokana na kuwa karibu na kwa makusudi yote na wanangu, na pia kupata muda wangu binafsi pia. Na pia kupakia vitu hapa ndio kumepata pigo kubwa zaidi, na kwa kweli sijielewi kabisa na hilo,” Namu alilalama.

Katika picha hiyo ya upendo wa baba kwa wanawe, watu wengi walivutiwa nayo na kumsifia kwa kujenga ukaribu na watoto wake wakiwa wachanga.

“Hivi ndivyo inakuwa ukikutana na mwanamke mzuri katika maisha yako,,sio ile burukenge ingine,,kila la kheri kaka,” Katoi Simon aliandika.

“Nzuri sana hii, na pia nampa heshima mama watoto kwa sababu umri kama huo umaweza ukamfanya mtu kuwa kichaa bila kujua,” Caroline Wairimu alisema.

“Inapendeza sana! uwe na uzoefu mzuri na ufikie kikubwa hakuna kisichowezekana katika ulimwengu huu, hata ulimwengu wenyewe unasema kuwa inawezekana,” John Lesepe alimtakia.