Amber Ray aanzisha vita dhidi ya kanisa la ADC kwa kumpigia kelele alfajiri 6am

Amber Ray alipakia video kwenye insastory yake akielezea kukerwa kwake na maandamano ya kanisa hilo.

Muhtasari

• Alisema kilichomchukiza ni kwamba wanapiga kelele asubuhi na wanachosema hata hakielewi.

Amber akerwa na kanisa kupiga kelele
Amber akerwa na kanisa kupiga kelele
Image: Instagram, Facebook

Mwanasosholaiti Amber Ray ameanzisha vita vikali mtandoani dhidi ya kanisa la African Divine Church, ADC la humu Kenya kwa kufanya maandamano alfajiri ya saa kumi na mbili wakipiga kelele.

Kwa wale hawajui, waumini wa dhehebu la ADC wanajulikana kwa kuzungumza mitaani wakiwa katika makundi ya watu kadhaa huku wanaimba, wakicheza densi na kucheza ngoma kwa mbwembwe zote.

 Sasa tabia hii yao inaonekana kumkera Amber Ray ambaye kupitia kwa ukurasa wake wa Instagram, alipakia video ambayo alichukua kutoka juu ya ghorofa anamoishi akisema kuwa waumini hao walimuamsha kwa kelele zao za kukera alfajiri na kumpotezea usingizi wa wikendi yake.

Amber Ray alisema kuwa anaheshimu sana dini lakini kwa itikadi kama hizo za ADC basi atakuwa ndio mwanzo anapoteza heshima yake kwao na hata kumtag gavana Sakaja kuchukua hatua madhubuti.

“Mimi naheshimu sana dini lakini hii ni mbaya kwa njia zote. Hii kelele yote asubuhi ya 6am na hivo sisi tuko katika ghorofa ya 7 na mbaya zaidi ni kwamba mimi hata sielewi wanaimba nini. Naapa hata sijawahi sikia klabu zikipiga kelele kiasi hiki. Gavana Sakaja, hii ni haki kweli?” Ray aliuliza.

Malalamishi ya Ray yanakuja kipindi ambapo kuna mjadala mkali nchini kuhusu baadhi ya makanisa kudhibitiwa kwa sauti za juu wanazozitoa wakati wa mahubiri yao jijini Nairobi.

Hii ni kufuatia hatua ya uongozi wa kaunti ya Nairobi kutoa amri kali kwa maeneo ya starehe kupunguza kelele zao au kufungwa na kunyang’anywa lleseni za kuhudumu – haswa klabu ambazo zinahudumu karibu na makazi ya watu.

Wiki jana gavana Sakaja alizungumzia pendekezo la kuendelezo amri hizo hadi kwa makanisa ambapo alisema maeneo ya kuabudu hayatazuiwa kwa njia yoyote katika kelele wanazopiga kwani ni za kuabudu Mungu.