Michelle Ntalami: Mimi si msagaji jamani, Wanaume mna nafasi ya kunitongoza!

"Kwa muda mrefu watu wamekuwa wakidhani ninavutiwa kwa wanawake, si kweli" - Ntalami.

Muhtasari

• Mjasiriamali huyo pia alikanusha madai kuwa anachumbiana kimapenzi na mwanamuziki Fena Gitu.

• Michelle na Gitu walionekana katika picha zenye ukakasi wiki jana, kuvutia uvumi kuwa huenda ni wapenzi.

N
N
Image: Instagram

Michelle Ntalami, mrembo mjasiriamali wa bidhaa za kujipodoa ameweka wazi kuhusu uhusiano wake na mwanamuziki Fena Gitu, kufuatia picha zao za pamoja zenye ukakasi mwingi zilizosambaa mitandaoni wiki jana.

Wengi ambao walichanganua picha hizo walihisi kuwa huenda wawili hao ni wapenzi wasagaji kwa jinsi walivyokuwa lakini Ntalami amekanusha madai hayo vikali huku akisema Gitu kwa muda mrefu amekuwa rafiki wa karibu ambaye wameshirikiana naye katika kufanikisha mambo tumbi nzima.

“Chenye naweza sema ni kwamba Fena ni rafiki mmoja mzuri sana kwangu na hakuna kinachoendelea kimapenzi baina yetu. Kwa wale ambao wanatujua au pengine tumewahi kutana nao mnaweza gundua kuwa urafiki wangu na Fena ulianza kutoka Instagram, tumefanya miradi mingi pamoja. Tumefanya video za muziki naye, amekuwa balozi wa mauzo kwa bidhaa zangu kwa muda mrefu tu,” Ntalami alisema katika mahojiano na kituo kimoja cha redio humu nchini.

Mrembo huyo pia alikanusha madai kuwa yeye ni msagaji huku akisema kwa mara kadhaa hapo awali alilazimika kuliweka wazi hilo kwamba yeye si msagaji bali ni mtu ambaye ana mvuto wa aina yake kwa jinsia ya kiume kwa kimombo ‘androsexual’

Alisema kuwa wanaume wote wako na nafasi ya kujaribu bahati yao katika kumtongoza kwani yeye nguzi za nguvu zake zinavutia upande huo.

“Nimewahi lizungumzia hilo kwamba mimi si msagaji bali nina mvuto kwa watoto wa kiume na nyuzi zinavutia upande huo. Kwa hiyo wanaume wanaweza jaribu bahati yao kwa sababu hicho ndicho kinanivutia. Watu wamekuwa wakinidhania kuwa navutiwa kwa wanawake lakini huo si kweli,” Michelle Ntalami alisema.

Mwaka jana, Ntalami alijipata katika jungu la gumzo kali kumhusisha na usagaji baada ya kuonekana katika sehemu mbalimbali na mwanaharakati wa wanajamii wa LGBTQ nchini Kenya, mwanahabari Makena Njeri ambaye alitangaza waziwazi kuwa yeye ni msagaji.

Baadae zilivuma habari kuwa Ntalami amemuacha Makena Njeri katika kile kilichotajwa kuwa ni usaliti na kuchepuka, jambo oambalo ukweli wake haukubainika bayana mpaka lilipofifia na kutoweka kwenye mwanga.