Zari Hassan na Shakib wafunga harusi ya Kiislamu kisiri baada ya kuvishana pete (Video)

Harusi hiyo ilifanyiwa chumbani ambapo watu wachache walihudhuria na katika video Shakib anaonekana akimvisha Zari pete.

Muhtasari

• Inaarifiwa baada ya sherehe hiyo, Zari na Shakib waliweka kila kitu wazi kwa wazazi wa Zari.

Zari Hassan na Shakib wafunga harusi ya kisiri.
Zari Hassan na Shakib wafunga harusi ya kisiri.
Image: Screengrab

Mjasiriamali na mwanamitindo maarufu kutoka Uganda Zari Hassan kwa mara nyingine tena amevishwa pete ya uchumba na mpenzi wake wa muda Shakib Lutaaya.

Wawili hao walivishana pete usiku wa manane kuamkia Jumatatu katika hafla ya faraghani ambayo ilihudhuriwa na idadi ndogo ya watu.

Katika picha na video ambqazo zimeenezwa kutoka kwa hafla hiyo iliyofanyika chumbani, wapenzi hao wanaonekana wamevalia Kiislamu kabisa huku wote wakiwa wameketi kwenye mkeka uliotandikwa sakafuni.

Shakib anaonekana akiinama kwa goti moja na kumvisha Zari pete ya uchumba kwa furaha kabla ya wawili hao kupigana mabusu waliohudhuria wakiwasherehekea kwa makofi.

Vyanzo vya habari kutoka Uganda vilidai kwamba baada ya kuvishana pete katika tukio la farahani, wawili hao waliweka Nikkah yao bayana kwa wazazi wa Zari.

Zari mwenye umri wa miaka 42 amekuwa akitupiwa maneno ya lawana na baadhi ya watu kwa kuchumbiana na mwanamume mdogo kiumri, lakini hilo halijakuwa kikwazo hata kidogo katika mapenzi yao.

Mfanyibiashara huyo ambaye ni mzazi mwenza wa msanii Diamond Platnumz aliwasuta wale wanaomsema kwa kuchumbiana na Shakib, akidai kuwa mbona suala la umri si kikwazo wakati mwanamume mkubwa anapotoka kimapenzi na mwanamke mdogo lakini ikigeuka upande mwingine huwa ni gumzo kubwa.

Zari, mama wa watoto watano amekuwa akichumbiana na wanaume mbalimbali tangu kifo cha mumewe wa ndoa Ivan Semwanga.

Alikuwa katika mapenzi na msanii Diamond Platnumz kabla ya kuachana 2018 na baadae mwaka 2022 alionekana na mwanamume mdogo aliyetambulika kwa jina GK Choppa lakini mapenzi yao hayakuchukua muda mrefu.

Baadae mwaka huo huo alianza kuonekana na Shakib Lutaaya ambaye wamedumu kwa miezi kadhaa pamoja mpaka kuvishana pete za uchumba usiku wa Jumapili katika sherehe ya Kiislamu.

Kuvishana pete na kijana mdogo kunakuja wiki moja tu baada ya mfanyibiashara Akothee ambaye anafananishwa kwa mambo mengi tu kufunga harusi ya kifahari pia na mpenzi wake mdogo, Mzungu Denis Schweizer, aliyempa jina Mr Omosh.