Shakib Cham adhibitisha kufunga Nikkah na Zari Hassan, "wawili ni bora kuliko mmoja!"

Shakib amekuwa gumzo kwa kuchumbiana na Zari, mama wa miaka 42 ambaye ana watoto 5 tayari kutoka kwa wanaume tofauti.

Muhtasari

• Lutaaya alinukuu kifungu cha Qur’an kwamba imeandikwa wawili ni sawa kuliko mmoja.

• Jumatatu Radio Jambo iliripoti kwamba Zari Hassan na Shakib Lutaaya hatimaye walifunga ndoa ya Kiislamu almaarufu Nikkah.

Shakib adhibitisha kufunga ndoa ya Kiislamu na Zari Hassan.
Shakib adhibitisha kufunga ndoa ya Kiislamu na Zari Hassan.
Image: Instagram//ShakibCham

Shakib Cham Lutaaya, mpenzi wa mwanamitindo na mfanyibiashara Zari Hassan amevunja kimya baada ya kudaiwa kufunga harusi ya Kiislamu katika hafla ya faraghani na mama huyo wa watoto watano.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Lutaaya alipakia video yenye tukio zima lililofanyika ndani ya nyumba faraghani na kuwaonesha wawili hao wakivishana pete mbele ya watu wa karibu.

Lutaaya alinukuu kifungu cha Qur’an kwamba imeandikwa wawili ni sawa kuliko mmoja.

“Na tuliwaumba kwa makundi makundi, Qur’an 78:8,” Lutaaya alinukuu.

Jumatatu Radio Jambo iliripoti kwamba Zari Hassan na Shakib Lutaaya hatimaye walifunga ndoa ya Kiislamu almaarufu Nikkah baada ya kuchumbiana kwa takribani mwaka mmoja.

Wawili hao walivishana pete usiku wa manane kuamkia Jumatatu katika hafla ya faraghani ambayo ilihudhuriwa na idadi ndogo ya watu.

Katika picha na video ambazo zilienezwa kutoka kwa hafla hiyo iliyofanyika chumbani, wapenzi hao wanaonekana wamevalia Kiislamu kabisa huku wote wakiwa wameketi kwenye mkeka uliotandikwa sakafuni.

Shakib alionekana akiinama kwa goti moja na kumvisha Zari pete ya uchumba kwa furaha kabla ya wawili hao kupigana mabusu waliohudhuria wakiwasherehekea kwa makofi.

Vyanzo vya habari kutoka Uganda vilidai kwamba baada ya kuvishana pete katika tukio la farahani, wawili hao waliweka Nikkah yao bayana kwa wazazi wa Zari.

 

Zari amekuwa akichumbiana na wanaume ainati tangu kuachana na msanii Diamond Platnumz mwaka 2018.

Zari mpaka kuachana na Platnumz walikuwa wamebarikiwa na watoto wawili ambao wanaishi na mama yao na wazazi hao wanashirikiana kwa kuwalea, huku Diamond akitembelea familia hiyo Afrika Kusini na wakati mwingine Zari akija Tanzania na watoto hao kwa baba yao.