Mimi sikuwahi mtafuta Vera Sidika, yeye ndiye alikuwa ananiandama - Otile Brown

Otile Brown alikanusha vikali kwamba Vera Sidika aliwahi msaidia kulipa bili za matumizi yake ya kimaisha akisema kwamba hakuna mwanamke aliyewahi kumlipia bili yoyote.

Muhtasari

• Msanii huyo alifunguka kwamba si yeye alimtafuta na kumtongoza Vera Sidika bali mwanasosholaiti huyo mstaafu ndiye aliyemfuata.

Otile Brown
Otile Brown
Image: Screengrab

Msanii wa kizazi kipya, Otile Brown amefunguka jinsi mahusiano yake ya kimapenzi yalivyoanza na mwanasoshoaiti Vera Sidika.

 Akizungumza na Oga Obinna kwenye chaneli yake, Brown alifichua kwamba kipindi wanaanza mahusiano na Vera Sidika, alikuwa anaishi sehemu za Ruaka.

Msanii huyo alifunguka kwamba si yeye alimtafuta na kumtongoza Vera Sidika bali mwanasosholaiti huyo mstaafu ndiye aliyemfuata.

Brown alisema kwamba kwa kipindi kirefu alijaribu kumkwepa lakini aliyekuwa meneja wake kipindi hicho, Noriega akamtaka kuchukua simu yake kumsikiliza kwani Vera alikuwa anamsumbua kwa simu mara kwa mara.

“Mimi sikumfuata, alinitafuta sana. Nafikiri aliingia kwa DM yangu lakini yeye ndiye alikuwa ananipigia simu sana. Vera ni mtu mzuri sana na nampa maua yake. Yeye ndiye alikuwa ananitafuta sana. Kusema ukweli Noriega ndiye mtu aliyeniambia kwamba msikilize,” Otile Brown alisema.

“Nakumbuka nilikuwa nilifanya shoot ya video ya ‘Chaguo la Moyo’, Vera Sidika alikuwa anapiga simu yangu mara kwa mara nikiwa location. Kwa hiyo wakati nilipokea simu aliniambia ‘Niaje, unaweza tokea. Kuja kwa Spa yangu. Nikatokea hapo na, ilikuwa vizuri. Sitaki kusema kwamba nilikuwa katika mapenzi lakini kile ninachojua ni kwamba Vera ni mtu amazing sana,” aliongeza.

Otile Brown alikanusha vikali kwamba Vera Sidika aliwahi msaidia kulipa bili za matumizi yake ya kimaisha akisema kwamba hakuna mwanamke aliyewahi kumlipia bili yoyote na hilo halitawahi tokea katika maisha yake.

Msanii huyo akizungumzia uwepo wa Vera Sidika kwenye wimbo wake ‘Baby Love’ kama vixen, alisema kwamba maudhui ya wimbo wenyewe hajakuwa kumhusu Vera bali mrembo huyo mama wa watoto wawili kwa sasa ndiye aliupenda wimbo na kutaka kuwepo kwenye video.

“Wimbo haukuwa kuhusu Vera. Nafikiri alipenda wimbo na kuniomba awepo kwenye video. Nilipotoka kwa studio na ngoma hiy0, nilienda kwa salon yake nikamchezea na aliipenda hapo hapo na kuniomba kuwepo kwenye video,” Otile Brown alisema.

Hata hivyo, mwaka 2018 baada ya kuachana na kurudiana baada ya muda mfupi, Vera katika mahojiano aliwahi kiri kwamba msanii huyo hakuwa na mapenzi ya dhati kwake bali alimtumia tu ili kupata mvuto zaidi kwenye muziki wake.

Vera katika mahojiano yake kwenye stesheni moja ya redio nchini kipindi hicho, alisema kwamba alikubali kumrudia Otile Brown baada ya msanii huyo kumbembeleza.

"Alikuwa ananibembeleza [turudiane] kwa muda wa kama wiki mbili hadi tatu na nikasema labda amegundua makosa yake na mimi ni mtu ambaye ninaamini sana katika kumpa mtu nafasi ya pili baada ya kukosea," Vera alisema.