Rev Lucy Natasha azungumzia alichojifunza kutokana na kifo cha TikToker Brian Chira

"Hebu tuweni na nguvu sawia, zile nguvu ambazo watu hutumia kuchangisha wakati mtu amekufa, tuzitumie kufanikisha maisha ya watu wakiwa hai, acha tuwafanye wajue kuwa tunawathamini."

Muhtasari

• Brian Chira alifariki mwezi mmoja uliopita katika ajali ya barabarani baada ya kugongwa na gari majira ya alfajiri akisemekana kuwa alikuwa anatoka katika mtoko wa tafrija.

• Baada ya kifo chake, jamii ya tiktokers waliungana pamoja kwa idadi kubwa na kuchangisha Zaidi ya shilingi milioni 8 kwa ajili ya mazishi yake.

Lucy Natasha azungumzia mafunzo kutoka kwa kifo cha Chira
Lucy Natasha azungumzia mafunzo kutoka kwa kifo cha Chira
Image: Screengrab (Obinna TV), Maktaba

Mchungaji Lucy Natasha wa kanisa la Empowerment Christian Church, ECC amezungumza kwa mara ya kwanza mambo aliyojifunza kutokana na kifo cha tiktoker Brian Chira.

 Natasha ambaye alikuwa katika Obinna Show Live kwenye YouTube, alisema kwamba alimfahamu Brian Chira kutokana na TikTok na anahisi kifo chake kilikuwa ni umauti wa mapema ambao haukutarajiwa.

Alisema pia kwamba kifo cha Chira kilifunua mengi katika kizazi cha sasa kwamba watu wanaweza kudhihaki ukiwa hai lakini ukifa wanajumuika pamoja kuchanga mamilioni ya pesa kwa ajili ya kufanikisha msiba wako.

Natasha pia anahisi kwamab kifo cha Chira kilimfungua macho kugundua kwamba watu wengi wakiwa hai huwa hawapati nafasi ya kukabidhiwa koja lao la maua, hadi pale wanapofariki maua ghali yanapandwa kwenye makaburi yao.

“Mimi nahisi haya ni maisha ambayo yalipotea mapema sana na kwa ghafla mno, unajua hili ni tukio ambalo pengine lingezuilika kutokea, lakini mafunzo machache ambayo ninaweza chukua kutoka kwa kila kitu ambacho kilizingira kifo chake, na ambacho si sahihi hata kwenye jamii yetu ni kwamba watu wanaweza jumuika pamoja, wachangishe pesa na kukuzika, lakini watu hawawezi ungana pamoja wachangishe pesa kufanikisha ndoto yako,” Mchungaji Natasha alisema.

“Na kitu kingine ambacho kizazi cha sasa hakifanyi, huwa hatumpi mtu maua yake akiwa hai, hatuwasherehekei wakiwa hai, ni kama ili mtu kusherehekewa unafaa ufe kwanza. Na nahisi kabisa hilo si sahihi. Fikira zangu ni kwamba tunastahili kubadilisha jinsi tunavyochukulia mambo, kama jamii, kama kizazi, hebu na tuwape watu maua yao wakiwa hai, tuwasherehekee, na pia hebu tuweni na nguvu sawia, zile nguvu ambazo watu hutumia kuchangisha wakati mtu amekufa, tuzitumie kufanikisha maisha ya watu wakiwa hai, acha tuwafanye wajue kuwa tunawathamini,” mchungaji huyo aliongeza.

Brian Chira alifariki mwezi mmoja uliopita katika ajali ya barabarani baada ya kugongwa na gari majira ya alfajiri akisemekana kuwa alikuwa anatoka katika mtoko wa tafrija.

Baada ya kifo chake, jamii ya tiktokers waliungana pamoja kwa idadi kubwa na kuchangisha Zaidi ya shilingi milioni 8 kwa ajili ya mazishi yake.