“Unanipenda au unanitumia tu?” Zuchu amuuliza Diamond, ataka kujua ndoa ni lini (video)

Kufuatia maswali yake ya kijanja, mashabiki waliohudhuria walifurahishwa na kumuunga Zuchu mkono kwa swali lake kwa Diamond kuhusu ndoa na kuanza kuradidi “Muoe! Muoe! Muoe!”

Muhtasari

• Moja kati ya tumbuizo lililozua gumzo Zaidi mitandaoni ni pale Zuchu na Diamond walipopanda jukwaani kwa ajili ya kutumbuiza wimbo wao wa pamoja ‘Mtasubiri sana’.

• Wakati huo huo, Diamond naye alimuimbia akimuuliza maswali hay ohayo na pia kutaka kujua Zuchu atamzalia lini.

Diaond na Zuchu kwenye ubora wao jukwaani.
Diaond na Zuchu kwenye ubora wao jukwaani.
Image: Screengrab//WasafiMedia

Usiku wa Jumanne, asilimia kubwa ya wasanii wa Tanzania walijumuika katika mkoa wa Tanga wilayani Pangani kwa ajili ya Mkesha wa Mwenge.

Katika hafla hiyo ya tafrija, wasanii mbalimbali walipanda jukwaani na kuwatumbuizia mashabiki kwa nyimbo zao pendwa.

Moja kati ya tumbuizo lililozua gumzo Zaidi mitandaoni ni pale Zuchu na Diamond walipopanda jukwaani kwa ajili ya kutumbuiza wimbo wao wa pamoja ‘Mtasubiri sana’.

Katika wimbo huo ambao upo kama shiri la ngonjera, wawili hao ambao pia wamekuwa wakitajwa kama wapenzi waliimbiana kwa zamu mistari ya kuulizana maswali kuhusu mapenzi yao.

Zuchu aliushangaza umati baada ya kuchombeza maneno yake ya kibunifu akimuuliza Diamond kama anampenda kweli na pia kwenda ndani Zaidi akitaka kujua ni lini Diamond atamuoa rasmi kwa ndoa ya Nikkah.

Wakati huo huo, Diamond naye alimuimbia akimuuliza maswali hay ohayo na pia kutaka kujua Zuchu atamzalia lini.

“Unanipenda mimi? Utanioa lini? Au unanitumia?” Zuchu alimuuliza Diamond.

 “Unanipenda mimi? Unaniamini? Utanizalia lini?” Diamond alimjibu Zuchu kwa kutumia maswali pia.

Kufuatia maswali yake ya kijanja, mashabiki waliohudhuria hafla hiyo walifurahishwa na walionekana kumuunga Zuchu mkono kwa swali lake kwa Diamond kuhusu ndoa.

Walifanya kama kiitikio wakiradidi “Muoe! Muoe! Muoe!” huku Zuchu akiwarushia noti za pesa kutoka jukwaani.

Wakiwa wapenzi, wawili hao bado hawajafunga ndoa licha ya tetesi kutoka kwa wazazi wao kudai wawili hao wanachezea saikolojia za mashabiki tu.

Hii hapa video ya Zuchu na Diamond jukwaani kwenye mkesha wa Mwenge, Pangani, mkoa wa Tanga: