Bahati azindua rasmi kampeni za kuwania ubunge wa Mathare

Muhtasari

•Mgombea ubunge huyo kwa tikiti ya Jubilee alionekana akizuru maeneo mbalimbali ya Mathare.

•Msanii huyo mwenye umri wa miaka 29 amekuwa akijipigia debe kutumia kauli mbinu "Kesho Yetu ni Leo".

Bahati na mbunge wa Kieni Kanini katika makao makuu ya Jubilee, Nairobi
Bahati na mbunge wa Kieni Kanini katika makao makuu ya Jubilee, Nairobi
Image: INSTAGRAM// BAHATI

Mwanamuziki Kelvin Kioko almaarufu Bahati ameanza rasmi shughuli ya kujipigia debe katika eneo la Mathare ambalo anatazamia kuwakilisha.

Katika kanda ya video ambayo alipakia Instagram, mgombea ubunge huyo kwa tikiti ya Jubilee alionekana akizuru maeneo mbalimbali ya Mathare.

Akiwa ameandamana na kikundi kikubwa cha vijana, Bahati alitembea maeneo kama sokoni, uwanjani na mitaani.

"Siku Yangu ya Kwanza kwenye Kampeni kama Mbunge Ajaye wa Mathare. Mtaa imeamua ni Time Ya Mtoto Wa Mathare!!! Bahati kwa Mbunge wa Eneo bunge la Mathare 2022," Bahati aliandika.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 29 amekuwa akijipigia debe kutumia kauli mbinu "Kesho Yetu ni Leo".

Alitangaza kujitosa kwake kwenye siasa takriban wiki mbili zilizopita katika makao makuu ya chama cha Jubilee ambacho anatazamia kutumia kuwania kiti.

Mapema mwezi huu, Bahati alimshirikisha kinara wa ODM, Raila Odinga katika ngoma ya kisiasa 'Fire'.