Rose Muhando akumbuka safari ngumu ya kupata afueni alipokuwa akiugua sana nchini Kenya

Muhando ameweka wazi kuwa sasa yupo sawa na kuwashukuru waliomshika mkono alipokuwa akiugua.

Muhtasari

•Mwaka wa 2017 mwimbaji huyo alifichua kwamba alikuwa akiugua ugonjwa usio wa kawaida ambao ulisababisha miguu yake kuvimba. 

•Kuugua kwa Muhando kulifichuka hadharani baada ya video ya Ng'ang'a alimfanyia maombi kusambaa mitandaoni.

Rose Muhando

Mwimbaji mkongwe wa nyimbo za injili Rose Muhando alikuwa aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa Ijumaa, Julai 29.

Muhando ambaye amekuwa akitumbuiza kwa takriban miongo miwili alitumia fursa hiyo kuwashukuru wote ambao walifanikisha kupona kwake alipokuwa akiugua vibaya takriban miaka minne iliyopita.

Mwaka wa 2017 mwimbaji huyo alifichua kwamba alikuwa akiugua ugonjwa usio wa kawaida ambao ulisababisha miguu yake kuvimba. 

Muhando ameweka wazi kuwa yupo sawa na kuwashukuru wote ambao walimshika mkono kipindi ambapo alikuwa akiugua.

"Shukurani za kipeke ziende Kwa watoto wangu @gift_gibson1 Nicolous na Maxmillian kwani walisimama na mimi nyakati zote na kunisapoti Kwa maombi na kunitia moyo bila kuchoka,Mungu awabariki sana, lakini kipekee shukurani zangu,ziende Kwa @annastaciakiatukivue @solomonmkubwa @official_neema_mwaipopo Kwani mlipitia magumu kipindi chote nilichougua nchini kenya ,mlipambana Kwa nguvu zote kuhakikisha narejea kwenye afya yangu Mungu awakumbuke na vizazi vyenu, na ni kweli Leo naendelea vizuri, Asante sana @annambise864 @mamaafrica ambaye pamoja na Hali yangu kiuchumu ilipodhoofika wewe ulinishika mkono ukasimama nami," Muhando alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mwimbaji huyo alitoa shukran za kipekee kwa  wachungaji, wakristo na serikali ya Kenya kwa kumkubali na kumsaidia katika kipindi alichokuwa akiugua jijini Nairobi.

"Mlinionyeha upendo wa Kimungu," Amesema

Muhando alitoa shukrani za dhati kwa mhubiri mtatanishi James Ng'ang'a ambaye alimkaribisha na kumuombea kanisani mwake.

Kuugua kwa mwimbaji huyo kutoka Tanzania kulifichuka hadharani baada ya video ya Ng'ang'a alimfanyia maombi kusambaa mitandaoni.

"MUNGU AMKUMBUKE BABA YANGU APOSTLE MAINA NG,ANG,A ambaye huyu alifanyika sababu kubwa ya watu wote kufahamu kuwa nilikuwa mgojwa,mungu alikutumia wewe kuwafikishia ujumbe wa afya yangu Kwa watu,wakaomba,wakanisaidia, maproducer wote mlionisaidia kunishika mkono nikiwa Sina kitu mkononi," Muhando alisema.

Pia alimshukuru mchungaji maarufu wa Kenya Lucy Natasha kwa maombi aliyomfanyia katika kipindi hicho.

"Nikisema niwataje hapa siwezi maliza leo ila wote nawashukuru mlionisaidia maana isingekuwa rahisi kuiona siku ya leo na nimeongeza mwaka mwingine wa kuendelea kumtumikia Mungu alie hai," Alisema.

Muhando alikuwa amelazwa hospitalini hapa nchini Kenya baada ya kuugua, lakini haijawahi kufunguka wazi kilichokuwa kimempata huku akifutilia mbali uvumi wa uraibu wa dawa za kulevya.