Yesu wa Tongaren atangaza Pasaka yake hufanyika Julai, aeleza jinsi inavyoadhimishwa

Alidai kwamba watu wengi hutumia Pasaka 'kuandamana' huku wakiwa wamebeba miti.

Muhtasari

•Yesu wa Tongaren amepuuzilia mbali sherehe za Pasaka ambazo zinaendelea miongoni mwa Wakristo kote duniani.

•Alifichua kuwa kanisa lake linatambua Pasaka katika mwezi wa Julai ambapo wana namna yao ya kufanya mambo.

Yesu wa Tongaren
Image: HISANI

Mchungaji mwenye utata mwingi kutoka kaunti ya Bungoma, Eliud Simiyu almaarufu Yesu wa Tongaren amepuuzilia mbali sherehe za Pasaka ambazo zinaendelea miongoni mwa Wakristo kote duniani.

Akizungumza na Citizen Digital, Bw Simiyu ambaye anajitambulisha kama ni Yesu wa sasa aliweka wazi kwamba yeye na wafuasi wake hawatambui Sherehe za Pasaka zinazoendelea akizitaja kuwa mitindo ya wazungu.

"Mimi nawaonya wafuasi wafuasi wangu, sisi hii Pasaka huwa hatuitendi. Haikubaliki katika milango hii ya Yerusalemu," alisema.

Mwanzilishi huyo wa 'Kanisa la Yesu' alidokeza kuwa watu wengi kote duniani hutumia Pasaka kama wakati wa 'kuandamana' huku wakiwa wamebeba miti kama ishara ya kusulubiwa kwa Yesu Kristo.

Alifichua kuwa kanisa lake linatambua Pasaka katika mwezi wa Julai ambapo wana namna yao ya kufanya mambo.

"Hiyo Pasaka inapofanyika huwa tunasoma maandiko kutoka kitabu cha 12:21-28. Hiyo ndiyo Pasaka ya Mwalimu Yesu. Lakini hii ambayo imeandikwa kwa Baruku, kulingana na maandiko inasema tujihadhari tusije tukaiga mitindo ya watu wa nchi za kigeni," alisema.

Kwenye mahojiano ya awali na mtangazaji Massawe Japanni, Yesu wa Tongaren alikanusha madai kwamba alikuwa akiificha ili kuepuka kusulubiwa wakati wa msimu wa Pasaka.

 Alibainisha kuwa kusulubiwa kulitokea tu kwa Yesu Kristo wa asili, karne 20 zilizopita wakati wa ujio wake wa kwanza duniani.Alisema mambo yamebadilika sana na kusulubiwa ni kinyume na sheria ya ulimwengu wa sasa.

"Hiyo ilikuwa miaka 2000 iliyopita. Katika kizazi hiki cha sasa, hilo jambo limepitwa na wakati. Kila kitu kinachotendeka ni lazima kiwe chini ya sheria. Iwapo hakipo, itakuwa ni kuvunja sheria," alisema takriban wiki mbili zilizopita.

Baba huyo wa watoto wanane alitumia mstari wa Biblia katika kitabu cha Waebrania 9:27-28 kueleza kwamba ujio wa pili wa Yesu Kristo ulisemekana kuwa kwa minajili ya kuwachukua wale wanaomngoja wala sio kuwaokoa wale wenye dhambi kama ilivyokuwa katika kuja kwake mara ya kwanza.

"Kusulubiwa sasa naona haikubaliki kwa sheria ya Mungu. Hiyo iliisha," alisema.

Bw alifichua kuwa alizindua kanisa lake 'Kanisa la Yesu' mwaka wa 2009 na ameendeleza  injili kwa zaidi ya mwongo mmoja uliopita. Alisema kuwa kanisa lake lina manabii kumi na wawili pamoja na washirika wengine.