CHOPPER YA RAILA

Ndege ya Raila ilianguka baada ya kupaa mita 5 juu

Hakuna maafa yoyote yalipatikana kwani rubani na abiria wanne waliokuwa ndani ya Chopper ile wakati wa ajali walinusurika na majeraha kidogo.

Muhtasari

•Raila alikuwa ameandamana na Rais Kenyatta ili kuizindua  barabara ya Wagai-Akala.

•iNdege ilianguka ikiwa mita 5 juu lipojaribu kupaa ili kutengeneza nafasi ya ndege zingine kutua.

Ndege iliyombeba Raila Odinga
Ndege iliyombeba Raila Odinga
Image: Hisani

Ndege aina ya Chopper iliyokuwa imembeba Kinara wa ODM, Raila Odinga kutoka Kisumu kuelekea Gem ilianguka na kuharibika punde baada ya kumshukisha Raila siku ya Jumapili.

Hata hivyo, hakuna maafa yoyote yalitokea kwani rubani na abiria wanne waliokuwa ndani ya Chopper ile wakati wa ajali walinusurika na majeraha kidogo.

Akidhibitisha ajali hiyo kupitia ujumbe wa kuchapishwa, msemaji wa Raila, Dennis Onyango alisema kuwa chopper ile ilikuwa imemshukisha Raila katika shule ya msingi ya Kudho ila ikaangukaa ilipojaribu kupaa.

"Ndege, Bell 407, nambari ya utambulisho 5Y-PSM ilimshukisha Bw. Odinga katika shule ya msingi ya Kudho iliyoko Gem na ilipojaribu kupaa ili kutengeneza nafasi kwa ndege zingine ikaanguka" Bw Onyango alisema.

Aliendelea kutangaza kuwa hakuna maafa yoyote yaliyotokea kwani rubani na abiria wote wanne waliponea na majeraha kidogo tu.

"Bw Odinga aliendelea vyema na shughuli zake na rais Kenyatta kama ilivyokuwa imepangwa' Onyango aliongezea.

Ujumbe ulioandikishwa na rubani wa ndege hiyo, Cpt Julius Mwambanga katika kituo cha polisi cha Akala ulisema kuwa ndege hiyo ilikuwa imepaa mita tano tu juu wakati ilianguka.

"Ndege ilipokuwa imepaa mita tano juu ilianguka chini na kugeuka pande ya kushoto na kusababisha kuharibika kwa lota ya nyuma na lota kuu. Rubani hakuumia ila abiria wake, Peter Mbeka alilalamika kuwa na maumivu kwenye kifua chake ila hali yake ni sawa" Ujumbe huo ulisoma.

Raila alikuwa ameandamana na Rais Kenyatta ili kuizindua  barabara ya Wagai-Akala. Uhuru ataongoza sherehe ya kuadhimisha siku ya madaraka siku ya Jumanne katika uwanja mpya wa Kenyatta ulio pande ya Kisumu.