Kisumu: Hatimaye familia ya mwanaume aliyeaga miaka 8 iliyopita yaruhusiwa kumzika

Familia ya marehemu Ogada imemtaka Onunga kulipa ada ya chumba cha kuhifadhi maiti ambayo kwa sasa imefikia Sh800,000 toka Mei 2014

Muhtasari

• Familia ya mchuna kahawa maeneo ya Tinderet ambaye aliaga mwaka wa 2014 itaweza kumzika marehemu baada ya mahakama ya Kisumu kusuluhisha mgogoro wa shamba.

•Familia ya marehemu ilishindwa kumzika baada ya mzozo kuhusiana na shamba lao la uridhi lililo katika kijiji cha Tieng’re K’oranda kuanza walipoenda kumzika pale.

Vijana wabeba jeneza ambayo ina mwili wa Ogada baada ya kufukuliwa mwezi Mei 2017
Vijana wabeba jeneza ambayo ina mwili wa Ogada baada ya kufukuliwa mwezi Mei 2017
Image: The Star

Hatimaye familia ya mchuna kahawa maeneo ya Tinderet ambaye aliaga mwaka wa 2014 itaweza kumzika marehemu baada ya mahakama ya Kisumu kusuluhisha mgogoro wa shamba.

Mwili wa Barack Ogada Ouko umekuwa katika chumba cha kuhifadhi maiti kwa miaka nane tangu mwezi wa Mei mwaka wa 2014.

Familia ya marehemu ilishindwa kumzika baada ya mzozo kuhusiana na shamba lao la uridhi lililo katika kijiji cha Tieng’re K’oranda kuanza walipoenda kumzika pale.

Inadaiwa kuwa Bwana James Onunga aliandamana na maafisa wa polisi kudai kuwa shamba lile lilikuwa lake na kupelekea kurudishwa kwa mwili wa Ogada kwenye chumba cha kuhifadhi mili.

Miaka mitatu baadae familia ya Ogada iliweza kupokea amri ya mahakama ya kuweza kuzika marehemu shambani mle ila Onunga akiandamana na polisi kwa mara nyingine alienda na kufukua mwili ule baada ya miezi miwili.

Hata hivyo, siku ya Jumatano wiki iliyopita hakimu Winfred Onkunya aliamuru kuwa Onunga alikuwa ameshindwa kudhibitisha kuwa shamba lile ni lake kwa nafuu ya familia ya Ogada.

“Amri inapeanwa kuagiza kughairiwa kwa hati ya hatimiliki ya James Onunga na badala yake  kunadikishwa kwa jina la Francis Ago(Marehemu)” Uamuzi wa korti ulisema.

Licha ya familia ya marehemu kupata afueni kuhusiana na mgogoro wa shamba, ilisemekana kuwa ada ya chumba cha kuhifadhia maiti ilikuwa imefikia laki nane. Familia hiyo imemtaka Onunga kulipa ada ile pamoja na hasara ya vyumba vilivyobomolewa wakati mwili wa marehemu ulikuwa unafukuliwa.

Inadaiwa kuwa vijana walibomoa manyumba katika eneo hilo baada ya mwili kufukuliwa na kubakisha paa moja ambayo imekuwa kivutio kwa kuambaa na barabara ya Kisumu kuelekea Busia.