SIASA ZA 2022

Mbunge Cate Waruguru amtema rais Kenyatta na kurejea kwenye boma la naibu rais

Mwanasiasa huyo alisema kuwa mikutano zaidi ya 40 aliyofanya na wapiga kura wa kaunti yake ya Laikipia ilimsaidia kufanya uamuzi huo.

Muhtasari

•Baada ya kumtema naibu rais William Ruto mwezi Juni mwaka uliopita na kuhamia ngome ya rais Uhuru Kenyatta, Waruguru amefanya maamuzi ya kurejea tena 'nyumbani' akitaja kutoridhishwa na uendelezaji wa chama cha Jubilee.

•Waruguru alitangaza hadharani kuwa amehamia chama cha UDA kinachohusishwa na naibu rais na akaapa kujenga ofisi za chama hicho katika kaunti hiyo ya Laikipia.

Waruguru akihutubia waombolezaji Laikipia
Waruguru akihutubia waombolezaji Laikipia
Image: FACEBOOK//CATE WARUGURU

Ni dhahiri kuwa mwakilishi wa kina mama katika kaunti ya Laikipia Cate Waruguru ameamua kurejea kwenye boma aliyogura takriban mwaka moja uliopita.

Baada ya kumtema naibu rais William Ruto mwezi Juni mwaka uliopita na kuhamia ngome ya rais Uhuru Kenyatta, Waruguru amefanya maamuzi ya kurejea tenanyumbani'  akitaja kutoridhishwa na uendelezaji wa chama cha Jubilee.

Alipokuwa anahutubia waombolezaji kwenye mazishi iliyofanyika Laikipia, Waruguru alitangaza hadharani kuwa atamuunga mkono naibu rais kwenye uchaguzi mkuu mwaka ujao.

Mwanasiasa huyo alisema kuwa mikutano zaidi ya 40 aliyofanya na wapiga kura wa kaunti yake ya Laikipia ilimsaidia kufanya uamuzi huo.

"Mimi ni mwanamke mjanja ambaye huweka maskio yake wazi kuskiza vile watu walio hapa wanasema.Nimefanya mikutano zaidi ya arubaini na nikawaskiza hawa watu vizuri wakasema 'William Samoei Ruto tosha 2022'" Waruguru alisema.

Waruguru alitangaza hadharani kuwa amehamia chama cha UDA kinachohusishwa na Ruto na akaahidi wakazi kurejeshwa kwa manufaa waliyokuwa wakipata kutoka kwa naibu rais hapo awali kabla hajamtema mwaka uliopita.

"Nataka kusema kuwa simba wa kike Cate Waruguru sasa ako ndani ya UDA.. Kutoka wakati nilitoka kwa mtu wa 'wheel barrow' hawa wanawake hawajawahi kuonja pesa za William Ruto, hata ofisi zake bado hazijajengwa hapa. Sasa mwenye atatengeneza hayo maneno ni mimi" Waruguru aliendelea kusema.

Hapo awali Waruguru alikuwa ameeleza kutoridhishwa kwake na chama cha Jubilee akimkosoa sana katibu mkuu Raphael Tuju kwa kile alisema ni kueneza ugomvi dhidi ya viongozi wa eneo la mlima Kenya.