Mama apoteza watoto wawili midomoni mwa fisi waliomuacha na majeraha mabaya pamoja na majirani wengine wawili

Muhtasari

•Lugo Nyale 2, na Mbodze Nyawa 1, waliaga papo hapo wakati fisi hao waliwashambulia na kuwala.

•Mulongo alijaribu kuwanusuru wanawe kutoka mdomoni mwa fisi wale ila juhudi zake hazikufua dafu na hapo akaamua kuenda kutafuta usaidizi ila kwa bahati mbaya fisi wale walikuwa washaua watoto hao wakati majirani walifika

hyena
hyena

Habari na Shaban Omar

Watoto wawili wadogo walipoteza maisha yao na watu wazima watatu kujeruhiwa baada ya kushambuliwa na fisi katika kijiji cha Baisa, eneo bunge  la Kinango, kaunti ya Kwale.

Lugo Nyale 2, na Mbodze Nyawa 1, waliaga papo hapo wakati fisi hao waliwashambulia na kuwala.

Kulingana na mashahidi, watoto hao wawili walikuwa na mama yao Mulongo Tsimba ambaye alikuwa anachoma makaa kabla ya tukio hilo kutokea.

Bi Mulongo alijaribu kuwanusuru wanawe kutoka midomoni mwa fisi wale ila juhudi zake hazikufua dafu na hapo akaamua kuenda kutafuta usaidizi ila kwa bahati mbaya fisi wale walikuwa washaua watoto hao wakati majirani walifika.

Kufuatia hayo wakazi wa kijiji cha Baisa wakaamua kuwashambulia fisi wale na wakafanikiwa kuua mmoja ila huyo mwingine akaweza kutorokea kichakani.

Hata hivyo Bi Mulongo pamoja na majirani wawili Kalu Chiti 21 na Mutuku Mutinda 64 walipata majeraha mabaya walipokuwa wanapambana na wanyama hao. Walipelekwa katika hospitali ya Samburu ili kupokea matibabu.

Polisi kutoka Kinango walithibisha tukio hilo huku miili ya watoto walioaga ikipelekwa katika mochari ya Kinango.