Bobi Wine ampigia debe mbunge Babu Owino, ashauri Wakenya kujiandikisha kama wapiga kura

Wine amesisitiza kuwa ni muhimu sana kwa kila raia kudai haki yake ya kupiga kura.

Muhtasari

•Wine amewashauri Wakenya wote kujiandisha kama wapiga kura ili waweze kushiriki kwenye chaguzi kuu za mwaka ujao

•Babu kwa upande wake amemshukuru Wine kwa kumpigia debe na kusihi waliofikisha umri wa kupiga kura wajiandikishe huku akimhakikishia kuwa Wakenya wanampenda.

Image: INSTAGRAM// BABU OWINO

Aliyekuwa mgombeaji wa kiti cha urais nchini Uganda Robert Kyagulanyi Ssentamu almaarufu kama Bobi Wine ameshawishi Wakenya wote ambao wamehitimu umri wa kupiga kura kujitokeza kujiandikisha.

Kupitia kwa  video ambayo imepakiwa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii za mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Wine amesisitiza kuwa ni muhimu sana kwa kila raia kudai haki yake ya kupiga kura.

Wine amewashauri Wakenya wote kujiandisha kama wapiga kura ili waweze kushiriki kwenye chaguzi kuu za mwaka ujao.

"Natuma salamu kwa wat u wangu wa Kenya haswa wa Embakasi Mashariki ambako ndugu yangu Babu Owino anatoka. Nataka kuwakumbusha kuwa ni muhimu sana kudai haki yako ya kikatiba. Tafadhali jiandikishe na uhakikishe kuwa waweza enda kupiga kura" Wine alisema.

Mwanasiasa huyo ambaye alianza kama mwanamuziki amewasihi wakazi wa eneo la Embakasi Mashariki kumchagua tena Babu Owino kwenye chaguzi za mwaka ujao.

"Wakati utaenda kuchaguana, chagua ndugu yangu Babu Owino.Tufanye hivi na tudai haki yetu kabisa. Comrades Tibim! Comrades Tialala!" Wine alimalizia kwa kusema.

Babu kwa upande wake amemshukuru Wine kwa kumpigia debe na kusihi waliofikisha umri wa kupiga kura wajiandikishe huku akimhakikishia kuwa Wakenya wanampenda.

"Shukran sana kwa rais wa Jamhuri ya Uganda Bobi Wine kwa kusihi Wakenya wajiandikishe kama wapiga kura na kushauri watu wa Embakasi Mashariki kunipigia kura mwaka wa 2022. Tunakupenda sana H.E Babu Owino" Babu alisema kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Babu Owino anahudumu katika muhula wake wa kwanza bungeni baada ya kunyakua kiti cha ubunge cha Embakasi mwaka wa 2017.

Owino ambaye alipata umaarufu mkubwa wakati alihudumu kama rais wa muungano wa wanafunzi katika chuo kikuu cha Nairobi alinyakua kiti cha ubunge kupitia tikiti ya ODM baada ya kumbwaga chini mpinzani wake wa karibu Francis Mureithi wa Jubilee.

Hata hivyo siasa zake zimekabiliwa na pandashuka si haba na amekuwa akikosolewa sana haswa kutokana na tukio ambapo alimpiga risasi DJ Evolve mwaka uliopita.