Mfahamu Dr. Resila A. Onyango, Polisi wa kwanza mwanamke kupata shahada ya Uzamivu (PhD) nchini Kenya

Muhtasari

•Afisa huyo alipata shahada yake ya kwanza kutoka chuo kikuu cha Moi kabla ya kujiunga na huduma ya police mnamo mwaka wa 2003.

•Dk Resila amewahimiza wanawake kutoogopa kujiunga na Idara ya polisi huku akisema hatua hiyo huwafungulia milango mingine mingi.

DKT Resila A. Anyango
DKT Resila A. Anyango
Image: NPS

Idara ya Polisi nchini (NPS) imemsherehekea afisa msimamizi mkuu wa polisi Resila A. Onyango kwa kuwa afisa wa kwanza mwanamke  nchini Kenya kupata shahada ya Uzamivu (PhD).

Dk Resila ambaye kwa sasa ndiye Naibu Mkurugenzi wa mipango katika afisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi alipata PhD na Mphil yake katika Haki ya Jinai kutoka Chuo cha John Jay cha Haki ya Jinai - Chuo Kikuu cha City cha New York.

Afisa huyo alipata shahada yake ya kwanza kutoka chuo kikuu cha Moi kabla ya kujiunga na huduma ya police mnamo mwaka wa 2003.

Dk Resila ni mwangalizi wa kijeshi aliyefunzwa katika Kituo cha Kimataifa cha Majeshi ya Ulinzi ya Finland nchini Finland na Mpelelezi wa Uhalifu wa Ngono aliyefunzwa katika Chuo cha Kimataifa cha Kutekeleza Sheria nchini Botswana.

Idara ya Polisi imesema Resila alipata mafunzo ya polisi katika kituo cha mafunzo cha Kiganjo mnamo mwaka wa 2003 na akaibuka kurutu bora zaidi wa kike, fanikio ambalo lilimfanya kupokea tuzo la Cane of Honor ambalo alikabidhiwa na rais wa wakati huo Mwai Kibaki.

Dk Resila amewahimiza wanawake kutoogopa kujiunga na Idara ya polisi huku akisema hatua hiyo huwafungulia milango mingine mingi.