Wawili washtakiwa kwa mauaji ya wakongwe wanne walioshukiwa kuwa wachawi Kisii

Muhtasari

•Kufikia sasa, washukiwa tisa wameshtakiwa mahakamani kwa mauaji ya wakongwe wanne; Sindege Mayaka, Rael Okware, Agnes Moraa na Jemimah Mironga ambao waliuawa kinyama baada ya kushukiwa kuwa ‘wachawi’.

Afisa wa polisi awafunga pingu Nelson Tumbo (kulia) na Hesborn Gichana (kulia) baada ya kushtakiwa kwa mauaji ya vikongwe wanne
Afisa wa polisi awafunga pingu Nelson Tumbo (kulia) na Hesborn Gichana (kulia) baada ya kushtakiwa kwa mauaji ya vikongwe wanne
Image: ANGWENYI GICHANA

Washukiwa wengine wawili walishtakiwa siku ya Ijumaa kwa mauaji ya wanawake wanne wakongwe  ambao walidaiwa kuwa ‘wachawi’ katika kijiji cha Mbanda, Kaunti Ndogo ya Marani huko Kisii mnamo Oktoba 17.

Nelson Tumbo na Hesborn Gichana walikanusha mashtaka yote manne ya mauaji walipofikishwa mbele ya Jaji wa mahakama kuu ya Kisii Hellen Ougo.

Kufikia sasa, washukiwa tisa wameshtakiwa mahakamani kwa mauaji ya wakongwe wanne; Sindege Mayaka, Rael Okware, Agnes Moraa na Jemimah Mironga ambao waliuawa kinyama baada ya kushukiwa kuwa ‘wachawi’.

Washukiwa wengine; Brian Nyakundi, Peter Angwenyi, Chrispin Ogeto, Justine Morara, Ronald Onyonka, Amos Nyakundi, na kijana mwenye umri wa miaka 17 walishtakiwa hapo awali mbele ya hakimu Ougo na kunyimwa dhamana.

Tumbo na Gichana walikaa kimya huku Jaji Ougo akiwasomea mashtaka ambayo walikanusha na kuzuiliwa katika Gereza Kuu la Kisii hadi Machi 1 na 2 mwaka ujao wakati ambapo kesi hiyo itasikizwa.

Siku ya Alhamisi, Hakimu Ougo aliwanyima dhamana Brian Nyakundi, Peter Angwenyi, Chrispin Ogeto, Justine Morara, Ronald Onyonka, Amos Nyakundi kijana mwenye umri wa miaka 17 dhamana 

Familia zaa wahasiriwa kupitia kwa wakili John Khaminwa ambaye aliteuliwa na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya na upande wa mashtaka zilikuwa zimepinga kuachiliwa kwa washukiwa hao kwa dhamana.

Katika uamuzi wake siku ya Alhamisi, Jaji Ougo alisema baada ya kuchunguza mazingira ya wanawake hao wazee wanne waliuawa na kuzingatia maoni kutoka kwa mawakili wa waathiriwa, alikataa kuwaachilia kwa bondi.