KCPE 2021: Magata Bruce Mackenzie mwanafunzi bora kwa alama 428, Jinsi wanafunzi bora walivyofanya

Muhtasari

•Magata Bruce Mackenzie ameibuka mwanafunzi wa kwanza akijizolea alama 428 kati ya alama 500 zinazostahili.

Waziri George Magoha na PS wa masomo ya chekechea na masomo ya msingi Dkt Julius Juan katika makao makuu ya KNEC mnamo Machi 28, 2022.
Waziri George Magoha na PS wa masomo ya chekechea na masomo ya msingi Dkt Julius Juan katika makao makuu ya KNEC mnamo Machi 28, 2022.
Image: ENOS TECHE

Waziri wa elimu George Magoha hatimaye ameachilia matokeo ya mtihani wa KCPE 2021 ambao ulikamilika mapema mwezi huu.

Magoha alitangaza matokeo hayo mwendo wa saa saba adhuhuri ya Jumatatu katika makao makuu ya KNEC, Nairobi.

Magata Bruce Mackenzie ameibuka mwanafunzi wa kwanza akijizolea alama 428 kati ya alama 500 zinazostahili. Bruce alikuwa mtahiniwa katika shule ya msingi ya Gilgil Hills.

Mtahiniwa bora katika mtihani wa KCPE 2021 Bruce Mackenzie
Mtahiniwa bora katika mtihani wa KCPE 2021 Bruce Mackenzie
Image: HISANI

Momanyi Ashley Kerubo kutoka shule ya msingi ya Makini School ameibuka wa pili na alama 427.

Watahiniwa sita walikalia nafasi ya tatu kwa alama 426. Sita hao ni Kwoma Charity Bunyanzi kutoka Holy Family Misikhu, Mbugua Sharon Wairimu Muteti kutoka Emmanuel Academy, Muteti Shantel Ndinda kutoka Kitengela International School, Stanley Otieno Omondi kutoka Rofin Field Juniour Sec School, Wekesa Naomi wa White Star Academy na Kimani Ethan Karuga kutoka Stepping Stone Preparatory.

Watahiniwa wengine sita walipata alama 425. Sita hao ni Njeru Joel Juniour Musyoka kutoka shule ya msingi ya Nyagwa, Kirinya Muriuki Victor kutoka PCEA Boarding Primary School,Diana Rose Natolo, Kaberia Emmanuel Munene, Emmanuel Kiplang'at Ngetich wa Moi Primary School Kabarak na George Morris Otieno wa Hill School. 

Waziri George Magoha katika makao makuu ya KNEC mnamo Machi 28, 2022
Waziri George Magoha katika makao makuu ya KNEC mnamo Machi 28, 2022
Image: ENOS TECHE

Mwaka jana, Faith Mumo kutoka Shule ya msingi ya Kari Mwailu, kaunti ya Makueni aliibuka wa kwanza akijizolea alama 433. Alifuatwa kwa karibu na Nanzala Wesonga kutoka Shule ya Msingi ya Wasichana ya Chogoria ambaye alipata alama 432. Angel Murithi na Samuel Wanyonyi  walishikilia nafasi ya tatu na alama 431.

Jumla ya watahiniwa 1,225, 597 walikalia mtihani huo katika vituo 28, 248 mbalimbali vya mitihani kote nchini. Watahiniwa wa kiume walichukua asilimia 50.28 ilhali wa kike walikuwa asilimia 49.72.

Magoha amesema kwamba matokeo ya jumla katika mtihani wa mwaka huu yameongezeka ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Kiingereza ndilo somo ambalo watahiniwa wa KCPE 2021 walipita zaidi.

Masomo ya Kiingereza, Kiswahili, Social Studies yaliandikisha ongezeko katika matokeo ya jumla.