TSC yawasimamisha kazi walimu 6 walioonekana katika video ya watoto wakiigiza ngono

Mitei aliwaalika walimu hao kutoa maelezo yao ya utetezi kwa kuiandikia Tume ndani ya siku 21 kuanzia leo (Alhamisi).

Muhtasari
  • Hii ni kufuatia video ya mtandaoni inayowaonyesha walimu wakiwalazimisha wanafunzi kuiga tukio la ngono
Picha: KWA HISANI
Picha: KWA HISANI

Tume ya Huduma kwa Walimu(TSC) imewasimamisha kazi walimu watano na mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Itumbe DOK iliyoko Nyamache, kaunti ya Kisii.

Hii ni kufuatia video ya mtandaoni inayowaonyesha walimu wakiwalazimisha wanafunzi kuiga tukio la ngono.

Barua ya Februari 2 na kuandikiwa walimu na TSC ilieleza kuwa kuwalazimisha wanafunzi kujihusisha na vitendo hivyo ni ukiukaji wa Kifungu cha 9 (1) cha Kanuni za Maadili ya Walimu.

TSC ilisema wanafunzi sita ambao wote walikuwa katika darasa la 2 walikabiliwa na kiwewe, mateso ya kisaikolojia na aibu.

"Umesimamishwa kazi  kuanzia tarehe 2 Februari," barua iliyotiwa sahihi na E.J. Mitei kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TSC Nancy Macharia ilisoma kwa sehemu.

Zaidi ya hayo, walielekezwa kuondoka katika eneo la shule na kuendelea kuwa nje, na kupoteza likizo yao ya kila mwaka.

Mitei aliwaalika walimu hao kutoa maelezo yao ya utetezi kwa kuiandikia Tume ndani ya siku 21 kuanzia leo (Alhamisi).

Haya yanajiri baada ya polisi kuomba siku saba za kuwazuia walimu hao ili wakamilishe uchunguzi.

“Tulifanikiwa kuwawasilisha mbele ya mahakama kwa madhumuni ya kuomba siku 7 zaidi kuwazuilia huku tukiendelea kufanya uchunguzi,” alisema Kipkemoi.

Kulingana na afisa huyo wa polisi, walimu sita walikamatwa kisha wa saba alinaswa baada ya kuhojiwa zaidi.