Watoto wafariki kwa kukosa hewa ndani ya basi ya shule

Wanafunzi walimlalamikia mara kadhaa kuhusu jinsi walivyokosa hewa.

Muhtasari

•Mandala, alikuwa akiendesha basi kuwarudisha wanafunzi makwao baada ya kufungwa kwa shule wakati kisa hicho kilipotokea Julai 8, 2022.

•Msemaji wa polisi katika jimbo la Lagos, SP Benjamin Hundeyin, alithibitisha kisa hicho na kusema kuwa dereva amekamatwa.

Wanafunzi
Wanafunzi
Image: screengrab

Dereva wa basi la shule moja nchini Nigeria, Odunsa Mandala anashikiliwa na Polisi baada ya wanafunzi wawili kufariki huku wengine wakizimia kutokana na kukosa hewa wakiwa ndani ya basi katika eneo la Aguda, jimbo la Lagos.

Mandala, alikuwa akiendesha basi kuwarudisha wanafunzi makwao baada ya kufungwa kwa shule wakati kisa hicho kilipotokea Julai 8, 2022.

Wanafunzi walimlalamikia mara kadhaa kuhusu jinsi walivyokosa hewa lakini alidaiwa kupuuza hadi wakati baadhi yao walipozimia.

Inadaiwa kuwa, mara baada ya kuona hali hiyo, alichukua hatua ya kupiga simu kuomba msaada na ndipo wanafunzi walioathirika wakakimbizwa katika hospitali ya Randle iliyopo jimboni Lagos na baadae wawili wakapoteza maisha.

Msemaji wa polisi katika jimbo la Lagos, SP Benjamin Hundeyin, alithibitisha kisa hicho na kusema, “Ndio, dereva amekamatwa lakini watoto tayari wamepoteza maisha, ni huzuni.”

Alioneza, “Dereva wa basi la shule alipuuza malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa watoto aliokuwa akiwapeleka nyumbani kwamba hawakuwa wakijisikia vizuri, na baadhi ya watoto walipoteza fahamu na wawili walikufa.”

Aidha, Msemaji huyo amezitaka Shule zijitahidi kuongeza wigo katika kuajiri na kuzingatia kanuni za kazi ikiwemo kuongeza idadi ya vyombo vya usafiri.

Pia aliwataka wazazi kufanya ukaguzi wa kina wa shule za awali zile za msingi kabla ya kuwapeleka watoto wao pale.

Hospitali ya Randle iliyopo jimboni Lagos ambapo wanafunzi wawili walipoteza maisha mara baada ya kufikishwa hapo kwa matibabu ya kukosa hewa.