Mauaji ya ‘Sniper’, DPP apendekeza mashtaka ya mauaji dhidi ya washukiwa

Sniper’ alitoweka Desemba 2 mwaka jana kabla ya mwili wake kugunduliwa wiki mbili baadaye.

Muhtasari

• Mwanapatholojia wa serikali Johansen Oduor, aliyefanya uchunguzi huo, alisema Sniper alikuwa na alama kwenye shingo yake na alionyesha dalili za mtu aliyekosa oksijeni.

Marehemu Daniel Muthiani,
Image: HISANI

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) amependekeza washukiwa wawili kushtakiwa kwa mauaji ya mwanablogu Daniel Muthiani Bernard almaarufu Sniper katika kaunti ya Meru.  

Katika taarifa DPP alisema kuna ushahidi wa kutosha kuendeleza mashtaka ya mauaji dhidi ya Vincent Muriithi Kirimi almaarufu Supuu na Murangiri Kenneth Guantai almaarufu Tali.

‘Sniper’ alitoweka Desemba 2 mwaka jana kabla ya mwili wake kugunduliwa wiki mbili baadaye.

Washukiwa watano baadaye walikamatwa kuhusiana na mauaji hayo. Walijumuisha; Kenneth Mutua Gatiri almaarufu Gasigi, Fredrick Muruiki Kiugi aka Papa, Franklin Kimathi almaarufu Dudu Ras, Timothy Kinoti almaarufu Timo na Murangiri Kenneth Guantai almaarufu Tali.

Walinaswa mjini Meru na maafisa wa upelelezi kutoka idara ya Uchunguzi wa Mauaji ya DCI na kuzuiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi jijini Nairobi na Kiambu.

Uchunguzi na upasuaji wa mwili wa marehemu katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Marimanti ulibaini kuwa alifariki kwa kunyongwa.

Mwanapatholojia wa serikali Johansen Oduor, aliyefanya uchunguzi huo, alisema Sniper alikuwa na alama kwenye shingo yake na alionyesha dalili za mtu aliyekosa oksijeni.